Sisi sio wanyonge kwa Iran – Mwamnyeto

DUBAI:KIKOSI cha timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ kimewasili salama mjini Dubai, Falme za Kiarabu tayari kwa maandalizi ya mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya Iran, utakaochezwa Oktoba 14, 2025.
Akizungumza mara baada ya kuwasili, mchezaji wa kikosi hicho, Bakari Mwamnyeto, amesema licha ya Iran kuwa na nafasi ya juu katika viwango vya soka duniani, Taifa Stars haioni sababu ya kujiweka kama timu dhaifu.
“Tunajua Iran ni timu kubwa na iko juu kwenye viwango vya FIFA, lakini sisi si wanyonge. Tunakwenda kupambana kwa nguvu zote. Wataona vipaji vya Tanzania na ushindani wa kweli,” alisema Mwamnyeto.
Ameongeza kuwa wachezaji wote wako katika hali nzuri kiafya na kisaikolojia, na kwamba mchezo huo ni fursa ya kuonesha maendeleo ya soka la Tanzania kimataifa.
Kwa upande wake, Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Hemed Morocco, amesema maandalizi yanaendelea vizuri na mchezo dhidi ya Iran ni wa aina yake kwa sababu unatoa changamoto ya hali ya juu kwa kikosi chake.
“Tunautazama huu kama mchezo mkubwa na wa maana. Iran ni timu ngumu lakini tunauchukulia kama fursa kwa vijana wetu kupata uzoefu na kuonesha uwezo wao. Tuko tayari kupambana,” alisema Morocco.
Iran, inayoshika nafasi ya juu barani Asia, imekuwa miongoni mwa timu zinazoshiriki mara kwa mara fainali za Kombe la Dunia, hali inayoufanya mchezo huo kuwa kipimo kizito kwa Tanzania kuelekea mashindano yajayo ya kimataifa.