Afrika Mashariki

CECAFA mambo safi, wawezeshwa mamilioni

NAIROBI: BARAZA la Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) kupewa sh milioni 814 baada ya kuingia ubia na kampuni kubwa ya michezo ya kubashiri, Betika, ambayo sasa itakuwa mdhamini rasmi wa Kombe la Kagame la CECAFA 2025/2026.

Michuano ya Kagame 2025 inatarajiwa kuanza kupigwa Septemba 2-15 kupitia mdhamini mpya aliyetangazwa asubuhi ya leo Alhamisi jijini Nairobi.

Michuano hiyo itakayoshirikisha klabu 11 za nchi wanachama wa Cacefa itafanyika Dar es Salaam, huku Simba na Yanga zikichomoa kwa mara nyingine kutokana na kutingwa na ratiba ngumu ya michuano ya kimataifa.

Makamu wa Rais wa CECAFA, Paulos Andemariam, amesema ushirikiano huo ni hatua kubwa kwa maendeleo ya soka katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

“Tunafurahi kuingia ubia na Betika. Kupitia udhamini huu, tunapeleka mashindano haya makubwa katika zama mpya.

“Hii ni ishara ya nguvu ya ushirikiano kati ya soka na sekta binafsi, na inadhihirisha imani ya chapa kubwa kama hii kwa thamani na mustakabali wa mashindano ya CECAFA,” alisema Weldehaimanot.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Betika Group, Mutua Mutava, alisema: “Huu si udhamini tu bali ni tamko la imani kwa nguvu ya soka kuunganisha, kuhamasisha na kubadilisha jamii,”amesema.

Kwa mujibu wa makubaliano hayo, Betika itapata fursa ya kujitangaza kupitia majukwaa yote ya CECAFA, ikiwemo mabango viwanjani na kampeni za kidijitali.

Related Articles

Back to top button