Partey asaini Villarreal huku akikabiliwa na tuhuma za ubakaji

LONDON: KIUNGO wa kati wa zamani wa Arsenal Thomas Partey, anayekabiliwa na mashtaka matano ya ubakaji nchini Uingereza, Jana alikamilisha uhamisho wa kujiunga na klabu ya Uhispania ya Villarreal.
Mchezaji huyo wa kimataifa wa Ghana mwenye umri wa miaka 32, ambaye anakanusha madai hayo, alipewa dhamana ya masharti Agosti 5 baada ya kufika katika mahakama ya London kwa makosa matano ya ubakaji dhidi ya wanawake wawili na moja la unyanyasaji wa kingono dhidi ya mwanamke wa tatu.
Makosa hayo yanayodaiwa yalifanyika kati ya 2021 na 2022, alipokuwa mchezaji wa Arsenal.
Partey alishtakiwa Julai 4, siku nne baada ya kuondoka The Gunners mkataba wake ulipokamilika mwishoni mwa mwezi Juni.
Katika kutangaza kuwasili kwake, Villarreal alisisitiza kwamba wanaheshimu kanuni ya msingi ya dhana ya kutokuwa na hatia.
Taarifa ya klabu hiyo iliendelea: Mchezaji huyo anatangaza kwa nguvu zote kutokuwa na hatia na anakanusha tuhuma zote zinazotolewa dhidi yake.
“Klabu… inasubiri uamuzi wa mahakama, ambayo itakuwa na jukumu la kufafanua ukweli unaodaiwa dhidi yake.”
Partey anatarajiwa kufika katika mahakama ya Old Bailey mjini London Septemba 2.
Alijiunga na Arsenal kwa pauni milioni 45 (dola 60 milioni) kutoka Atletico Madrid Oktoba 2020.
Aliichezea The Gunners mara 52 msimu uliopita na kufunga mabao manne. Kwa ujumla Partey aliichezea klabu hiyo michezo 167, akifunga mara tisa. Pia ameichezea Ghana mara 51.
Villarreal