Kocha Singida: tunaenda kulipa kisasi kwa Simba

DAR ES SALAAM: KOCHA Mkuu wa Singida Black Stars, David Ouma, amesema kuwa kikosi chake kiko tayari kulipa kisasi dhidi ya Simba SC katika mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB baada ya kupoteza kwao kwenye Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
Mchezo huo wa nusu fainali unatarajiwa kupigwa Jumamosi, Mei 31, katika Uwanja wa Tanzanite Kwaraa, uliopo Babati, Manyara. Mshindi wa mchezo huu atatinga fainali na kukutana na Yanga, waliotangulia mapema.
Akizungumza baada ya kupoteza mchezo wa ligi dhidi ya Simba kwa bao 1-0, Ouma amesema timu yake imejifunza makosa na sasa inakwenda kuyarekebisha kwa kuiondosha Simba kwenye michuano hiyo mikubwa.
“Tumecheza nao kwenye ligi, wametushinda kwa bao 1-0, lakini sasa tunakutana nao tena katika nusu fainali. Huu ni mchezo tofauti, tumejipanga na tunaenda kupambana kuhakikisha tunawatoa kwenye mashindano,” amesema Ouma.
Kocha huyo pia ameweka wazi kuwa licha ya kupoteza mchezo wa ligi, anaamini timu yake ilicheza vizuri na walipata nafasi ya kuona mapungufu yanayohitaji kurekebishwa kabla ya kushiriki mashindano ya kimataifa msimu ujao.
“Tulicheza mpira mzuri, na hiyo ni ishara kuwa tunaweza kufanya makubwa. Kipigo hicho kimetufungua macho na kutuonyesha tunapopaswa kuboresha ili kuwa bora zaidi,” ameongeza Ouma.