Burudani

Steve Nyerere aahidi milioni 10 kwa Tuzo za Tanzania Event Planners Awards

DAR ES SALAAM:MSANIImaarufu wa vichekesho nchini na Mwenyekiti wa Mama Ongea na Mwanao, Steve Mengere almaarufu Steve Nyerere, ameahidi kutoa kiasi cha shilingi milioni 10 kwa ajili ya kumuunga mkono mwandaaji wa Tuzo za Tanzania Event Planners Awards 2025, Bi Magreth Mvellah.

Akizungumza wakati wa hafla ya utoaji wa tuzo hizo, Steve Nyerere alimsifu Magreth kwa juhudi kubwa za kuandaa tuzo hizo kwa mwaka wa pili mfululizo, akimtaka kuendelea na juhudi hizo pasipo kukata tamaa.

“Kwa hili mlilolifanya ni kubwa. Kama Mama Ongea na Mwanao tutakupa Milioni 10 kwa kukushika mkono katika shughuli kubwa ya usiku wa tuzo za waandaaji wa shughuli mbalimbali,” amesema Steve.

Akiendelea kusisitiza umuhimu wa sekta hiyo, Steve amesema kuwa ana mpango wa kuwaunganisha washehereshaji na Mkurugenzi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ili kujadili changamoto wanazokumbana nazo kuhusu ulipaji wa kodi. “Tunatamani shughuli hii ifanyike Mlimani City mara ijayo na kuwahusisha watu mashuhuri ili kuthamini mchango wenu,” ameongeza.

Steve pia aliwahimiza washehereshaji na waandaaji wa matukio kuacha tofauti zao na kushirikiana kwa pamoja ili kukuza kazi yao. “Mungu amekupa maono ya kuwapa zawadi watanzania. Anayekudharau leo, kesho atakusujudia kwa heshima kubwa,” amesema kwa kumtia moyo mwandaaji huyo.

Kwa upande wake, Mvellah ameeleza kuwa tuzo hizo ni endelevu na zimefanyika kwa mwaka wa pili sasa, zikiwa na lengo la kutambua na kuthamini mchango wa wasanii na wataalamu wa upangaji matukio nchini. “Tunatamani tuzo hizi zitambulike zaidi, na hata Waziri wa Biashara na Uchumi awe miongoni mwa wageni wa heshima katika misimu ijayo ili kuona mchango wetu katika sekta hii bunifu,” amesema.

Mvellah amesisitiza kuwa tuzo hizo zitakuwa zikifanyika kila mwaka ili kuleta ushindani wenye tija na kukuza sekta ya upangaji wa hafla na matukio kwa kiwango cha kitaifa.

Related Articles

Back to top button