Kocha Singida azipumzisha silaha mbili kwa ajili ya Simba

SINGIDA: Kocha Mkuu wa Singida Black Stars, David Ouma, amefanya uamuzi wa kimkakati kwa kuzipumzisha silaha zake mbili muhimu, beki wa kushoto Ibrahimi Imoro na mshambuliaji Jonathan Sowah, kwa ajili ya kuwaandaa kwa mechi zinazokuja dhidi ya Simba SC.
Wachezaji hao hawajaambatana na kikosi cha timu hiyo kilichoelekea Pemba kushiriki mashindano ya Kombe la Muungano, ambayo yanatarajiwa kuanza rasmi Alhamisi, Aprili 24, kwenye Uwanja wa Gombani, kisiwani humo.
Singida Black Stars inatarajiwa kufungua dimba dhidi ya JKU ya Zanzibar bila uwepo wa nyota hao wawili pamoja na kiungo wao mahiri Marouf Tchakei ambaye anauguza jeraha.
Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa Singida Black Stars, Hussein Massan, uamuzi wa kuwapumzisha Sowah na Imoro ni kwa nia ya kuwalinda dhidi ya majeraha huku wakijiandaa kuivaa Simba katika michezo miwili mikubwa moja ikiwa ni ya Ligi Kuu Tanzania Bara na mwingine wa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB.
“Hawatakuwa sehemu ya kikosi cha mashindano ya Muungano. Wamepewa mapumziko mafupi na watarejea kuungana na timu katika michezo ya ligi, Kwa upande wa Marouf, alipata majeraha kwenye mchezo dhidi ya Tabora United na atakuwa nje ya uwanja kwa takriban wiki mbili.” amesema.