Ligi Kuu

Kipa Fountain Gate kikaangoni

Kusubiri kamati ya maadili

BABATI: KIPA wa timu ya Fountain Gate FC, John Noble, amejikuta matatani baada ya uongozi wa klabu hiyo kumwandikia barua ya kumsimamisha kwa muda huku wakisubiri kikao cha kamati ya maadili kuamua hatma yake.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisa Habari wa klabu hiyo, Issa Liponda, Mbuzi, Noble aliondolewa kambini mara baada ya kupewa barua ya kusimamishwa, huku hatua za kinidhamu zikisubiriwa mpaka kamati husika itakapokutana.

“Kamati hukaa ndani ya saa 72 baada ya mechi. Tunatarajia itakutana saa chache zijazo kujadili suala lake. Hatutaki kuharakisha uamuzi bila kumsikiliza, ikibainika amefanya makosa, basi tutachukua hatua stahiki,” amesema.

Amesema kwa sasa, haijafahamika kama kipa huyo yupo nchini au amerudi kwao, kwani aliondoka kambini muda mfupi tu baada ya kupewa barua hiyo ya kusimamishwa. Hata hivyo, mkataba wa Noble na Fountain Gate unatarajiwa kumalizika mwishoni mwa msimu huu.

Wakati sakata hilo likiendelea, kikosi cha Fountain Gate kinaendelea na maandalizi ya michezo mitatu ya mwisho wa msimu. Watachuana na JKT Tanzania, kisha kusafiri kuwavaa Coastal Union, kabla ya kufunga pazia kwa kumenyana na Azam FC kwenye Uwanja wao wa nyumbani – Tanzanite, Kwaraa.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button