Kwingineko

FIFA iko makini na afya za wachezaji – Infantino

ATLANTA, Rais wa FIFA Gianni Infantino amesema shirikisho hilo linachukulia suala la afya na ustawi wa wachezaji kama jambo la msingi zaidi na kipaumbele kwa shirikisho hilo linalosimamia soka duniani baada ya wasiwasi kuhusu kupanua mashindano katika kalenda ambayo tayari ina michuano mingi.

Hii inakuja baada ya Chama cha wachezaji wa soka duniani FIFPRO, Ligi kuu ya Hispania LaLiga na umoja wa ligi za Ulaya ziliwasilisha malalamiko ya pamoja kwa mamlaka za Usimamizi za Umoja wa Ulaya mapema mwezi Oktoba, wakishutumu FIFA kwa “matumizi mabaya ya kalenda yake”.

Akizungumza na kituo cha Televisheni cha CNN cha nchini Marekani Infantino amesema wadau hao wa soka wana hoja nzuri lakini wanapaswa kuondoa hofu juu ya kupanuliwa kwa kombe la dunia la vilabu kwakuwa athari zake kwa wachezaji zimezingatiwa.

“Ni michuano itakayokuwa ikichezwa kila baada ya miaka minne. Mshindi wake atacheza mechi saba tu mpaka kuwa bingwa ambayo ni wastani wa ongezeko la mchezo mmoja na nusu tu kwa mwaka hivyo sioni hiyo athari kubwa” – amesema.

“Kinachotokea kwa sasa kwenye ulimwengu wa soka ni kwamba kuna mechi nyingi sana kwa timu chache na wachezaji wachache ambao labda wanafika fainali katika michuano yote jambo ambalo sio rahisi kuonekana siku hizi ” – aliongeza

“Lakini tuko makini sana kwenye kalenda na kuhusu afya za wachezaji. Namaanisha tunataka kufanya kila kilicho bora kwa wachezaji wawe kwenye ubora wao. Na ni kitu ambacho wachezaji pia huniambia, ni bora kucheza mechi kuliko mazoezi si ndio” – aliongeza.

Wakosoaji wanawasiwasi kuwa kuboreshwa kwa mara ya nne ya Kombe la Dunia la Vilabu la timu 32 na michuano mingine iliyopanuliwa itaongeza idadi ya mechi kila msimu na kuwaacha wachezaji wakiwa na muda mchache wa mapumziko.

Related Articles

Back to top button