Muziki

Mastaa wa injili Afrika kutua tamasha la uchaguzi

DAR ES SALAAM:MKURUGENZI wa Msama Promotion Alex Msama amesema mastaa wa muziki wa injili kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika wanatarajiwa kupamba tamasha la uchaguzi litakalofanyika baadaye mwezi huu katika mikoa 26 ya Tanzania.

Aidha, ameomba wadau, taasisi na makampuni kujitokeza kusapoti tamasha hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam leo Msama amesema kuna mastaa wa Afrika wanaopendwa Tanzania watapewa nafasi ya kuburudisha katika tamasha hilo litakaloenda sambamba na maombi ya kuombea viongozi wa taifa.

Amesema anatarajia kuwaweka hadharani watakaotumbuiza hivi karibuni huku akiomba wadau mbalimbali kujitokeza kufadhili kufanikisha tamasha hilo na kuwawezesha wananchi kuingia bure kushiriki maombi.

“Kuna wasanii kutoka Nigeria na mataifa mengine ambao tunatarajia kuwaleta watakaoshirikiana na wa hapa nyumbani kuburudisha. Tunahitaji kuwaombea viongozi wetu na taifa letu ili kusudi uchaguzi mkuu ujao uweze kufanyika kwa amani na utulivu,”amesema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Makanisa ya Pentekoste Tanzania (CPCT) Mchungaji Emmanuel Mwasota amesema maombi hao hayabagui dini wala kabila bali yanafungua milango kwa ajili ya watu kuungana na kuliombea taifa.

Amesema wamekuwa wakisikia na kuona namna mataifa mengine  yanakuwa na vurugu baada ya kumaliza uchaguzi, ndio maana wanahitaji kushirikiana kila mtu kwa imani yake kuinua nchi, kushikamana madhehebu yote kuombea amani ili uchaguzi upite salama.

Tamasha hilo litaanza na Dar es Salaam kisha baadaye wataenda mikoa mingine mbalimbali. Kuhusu wapi Msama amesema atatangaza hivi karibuni.

Related Articles

Back to top button