2024 ilimrejesha Manara kwenye soka

MWEZI Julai mwaka 2024 ilikuwa siku nzuri kwa wapenda soka nchini, hatimaye aliyekuwa msemaji wa klabu ya Yanga, Haji Manara alimaliza adhabu yake ya kufungiwa kujihusisha na mpira ndani na nje ya nchi.
Manara alifungiwa miaka miwili na faini ya Sh milioni 10 baada ya kukutwa na hatia ya kumkosea nidhamu Rais wa TFF, Wallace Karia wakati wa mchezo wa Fainali ya Kombe la Shirikisho Tanzania Bara wakati huo likijulikana kama Azam Sports Federation Cup (ASFC) kati ya Yanga SC dhidi ya Coastal Union, fainali iliyopigwa jijini Arusha.
kurejea kwake kulizua taharuki kwani wadau wengi wa soka walionekana kuridhishwa na utendaji wa kazi wa kijana aliyekuwa katika nafasi hiyo Ally Kamwe. Mapema Jumapili ya Julai 28, soka la Tanzania limeamka tena na uvumi na drama. Ali Kamwe, mkuu wa kitengo cha Habari na mawasiliano wa Young Africans, alitangaza kujiuzulu.
Tangazo ambalo liliwaacha wengi hususan mashabiki wa klabu hiyo mdomo wazi Mwamba Haji Manara amerejea katika nafasi yake na kijana huyo sasa hana kazi ndani ya Yanga. Mara paap kesho yake Ali Kamwe akarejea ikisemekana tena ni juhudi za dhati za viongozi wa Yanga kusalia na kijana huyo mwenye upendo na klabu na kipaji cha hali ya juu kuinenea klabu.
Haji Manara, jina linalojulikana kwa maneno yake yenye kutatanisha na mara nyingi yenye ubishi na njonjo, ni mtaalamu wa sanaa hiyo. Kurudi kwake kuliashiria kuwaka tena taa ya ushindani kati ya Simba na Yanga katika nyanja ya usemaji.
Kurudi kwa Manara kwenye soka la Tanzania kulileta matokeo tofauti. Wakati wengine wanamuona kama mtu anayeleta mgawanyiko, wengine wanaamini uwepo wake ni muhimu kwa ukuaji wa mchezo wa soka nchini.
Licha ya kureja kwake hakupata nafasi ya kuendelea na kazi yake kwani tayari Ali Kamwe aliziba pengo na hapo Haji Manara akalazimika kuwa mwanachama wa kawaida.