Africa

Tumejipanga kupambana nao-Ongala

Sehemu ya wachezaji wa Al Akhdar.

KOCHA Msaidizi wa Azam, Kally Ongala amesema klabu hiyo inakwenda Libya ikiwa na lengo la kushinda au kupata sare dhidi ya klabu ya Al Akhdar ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kwenye mchezo wa marudiano kombe la Shirikisho Afrika(CAF).

Akizungumza na Spotileo Ongala amesema kikosi kitaondoka Oktoba 6 kikiwa na wachezaji 25 na wamejiandaa kukwepa hujuma kutoka kwa wapinzani wao.

“Al Akhdar ni timu nzuri tumeifuatilia rekodi zake tangu msimu uliopita na sisi tumejipanga kuhakikisha tunapambana nao na kupata ushindi kwao na kama itashindikana basi hata sare lengo letu ni kuvuka hatua inayofuata,” amesema Kally.

Kocha huyo amesema maandalizi yanakwenda vizuri na wachezaji wao wote wapo katika hali nzuri kuelekea mchezo huo.

Kwa mujibu wa Ongala, Azam itaondoka ikiwa imebeba kila kitu chao yakiwemo maji ya kunywa na vitu vingine vya muhimu ambavyo anaamini vitawasaidia kuwa salama muda wote wakiwa Libya.

Azam FC itashuka dimbani Oktoba 8 kucheza na Al Akhdar mchezo wa raundi ya kwanza wa Kombe la Shirikisho Afrika.

Mchezo huo utapigwa uwanja wa Benina Martyrs uliopo Benina kilomita 19 kutoka jiji la Benghazi.

Related Articles

Back to top button