Serikali yamuhakikishia maisha kocha Stars
DAR ES SALAAM: NAIBU Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo, Hamisi Mwinjuma (Mwana FA) amemuhakikishia kocha wa Taifa Stars, Hemed Selemani Morocco kuendelea kubaki kwenye benchi la ufundi hadi kwenye fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON), Morocco 2025.
Amesema hawana mpango wa kutafuta kocha mwingine kwenda na timu hiyo katika fainali hizo na kumuamini Morocco kuendelea na majukumu yake katika fainali hizo.
“Tunaimani kubwa na makocha wetu wazawa na kitendo cha Morocco na wasaidizi wake, kuipeleka Stars AFCON hatuna haja ya kuwaondoa, niwahakikishie wataenda Morocco,” amesema Mwana FA.
Katika hatua nyingine Rais Samia Suluhu Hassan amewapongeza Taifa Stars na ameagiza timu hiyo kupata mwaliko wa kutembelea bungeni Februari, mwakani.
“Tukiwa katika majonzi na kazi ikiendelea katika kuwatafuta ndugu zetu ambao tunaamini bado wako hai kufuatia kuporomoka kwa jengo eneo la Kariakoo, ninawapongeza vijana wetu Taifa Stars kwa ushindi na kufuzu kushiriki Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025.
Mmeandika historia kwa Taifa letu, ikiwa ni mara yetu ya nne kufikia mafanikio haya makubwa katika kipindi cha zaidi ya miaka arobaini,
Hongera kwa kazi nzuri nyote tuliowapa dhamana kusimama na vijana wetu kukamilisha jukumu hili katika Wizara na Shirikisho la Mpira wa Miguu (TFF), Benchi la Ufundi na Watanzania wote kwa kuendelea kuipenda, kuithamini na kuipa hamasa,” amesema.
Samia amesema baada ya ushindi huo, anawataka wachezaji na benchi la ufundi kujikita katika maandalizi mazuri zaidi kwa mashindano yajayo.