Michezo ya SHIMIWI Tanga 2022>>>Majaliwa kuyafungua rasmi Oktoba 5

MICHEZO ya Idara na Wizara za Serikali (Shimiwi) imeanza rasmi Oktoba Mosi, 2022 kwenye viwanja mbalimbali jijini Tanga.
Pamoja na michezo hiyo kuanza , lakini Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ataifungua rasmi michezo hiyo Oktoba 5 kwenye Viwanja vya Mkwakwani jijini humo.
Michezo hiyo yenye kushirikisha watumishi wa umma pekee kutoka kwenye Wizara na Idara za Serikali, yanatarajia kushirikisha watumishi zaidi ya 1,000, yakiwa na lengo kubwa la kuwajengea afya njema, kuongeza umakini, busara na ushirikiano baina ya watumishi hao.
MICHEZO HUSIKA
Kwa mujibu wa Kamati tendaji ya Shimiwi yenye kusimamia na kuendesha mashindano hayo, yatashirikisha michezo ya soka, netiboli, kuvuta kamba, riadha, mbio za baiskeli, kurusha tufe, karata, bao, drafti na darts kwa wanawake na wanaume.
VIWANJA VYENYEWE
Kwa mujibu wa waandaaji, viwanja vitakavyotumika ni pamoja na Mkwakwani, Polisi Chumbageni, Bandari, Tanroads, Gymkhana, Shule ya Ufundi Tanga na shule za sekondari za Galanos, Usagara na Popatlal.
Michezo hiyo ina kaulimbiu ya kuhamasisha michezo kwa watumishi mahala pa kazi ipewe kipaumbele ili kuwa na wafanyakazi wenye afya njema na sio goigoi kazini. Kaulimbiu ya mwaka huu ni: “Michezo hupunguza magonjwa yasiyoambukiza na huongeza tija mahala pa kazi”… Kazi Iendelee.
UMUHIMU WA MASHINDANO
Serikali imeona umuhimu wa mashindano haya makubwa kwa kupanga yafanyike kila mwaka, ili kuwaweka watumishi wake mahala pa kazi kuwa timamu, wenye afya njema na bidii kazini na kuondoa magonjwa nyemelezi (yasiyoambukiza) yanayosababishwa na mfumo wa maisha.
Umuhimu mwingine ni watumishi kujifunza mbinu mbalimbali za utekelezaji wa majukumu kwa makini kutoka kwa watumishi wenzao, kutokana na kushiriki wakiwa wanatoka kwenye wizara na idara mbalimbali, ambapo inasaidia kuwafanya wawe makini warejeapo mahala pa kazi.
Kuongeza ufanisi kwenye kazi mbalimbali kutokana na washiriki wanatoka kwenye kada mbalimbali zinazoendesha ofisi za Wizara na Idara za serikali, ambazo kwa asilimia kubwa zinahudumia wananchi wa rika mbalimbali.
NIDHAMU
Kutokana na klabu zote zinazoshiriki kwenye mashindano haya zinaundwa na watumishi wa umma, tunategemea nidhamu ya hali ya juu ndani ya uwanja kwa michezo yote itakayoshindaniwa, na hakuna atakayependezwa na vitendo vya uvunjaji wa amani kama kupigana na hata kutoleana maneno yasiyo na staa baina ya wachezaji kwa wachezaji au wachezaji na waamuzi na hata wachezaji au viongozi wa klabu na viongozi wa Shimiwi.
Mbali na nidhamu ndani ya uwanja pia tunategemea vivyo hivyo nje ya uwanja, kwa washiriki kuwa na lugha nzuri, kuvaa mavazi ya staa wawapo kwenye kituo cha mashindano, maana kuwepo kwao huko ni sehemu ya vituo vyao vya kazi.
KANUNI ZA MASHINDANO
Shirikisho limetunga kanuni za mashindano haya kwa mujibu wa Katiba ya Shimiwi ya mwaka 2009 Sura ya III Ibara ya 19 (3), ambazo zitatumika kwa ajili ya kusimamia na uendeshaji wa mashindano hayo, kutokana na katiba mpya ya mwaka 2021 kutakiwa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), kufanyiwa maboresho zaidi, ambapo kanuni hizo zimezungumzia masuala mbalimbali yanayohusiana na ushiriki kwa ujumla.
Kwa mujibu wa kanuni hizo, klabu zinazoruhusiwa kushiriki mashindano haya ni zile wanachama hai wa shirikisho hilo zilizotimiza masharti ya Katiba kwa kusajiliwa kwa msajili wa vyama na klabu za michezo nchini chini ya kifungu Na. 28 cha kanuni za Usajili za mwaka 1999.
Kanuni zimeeleza wazi kila klabu shiriki kwenye mashindano haya zitatakiwa kuthibitisha ushiriki wao kwa kuandika barua ikionesha ikitaja aina ya michezo itakayoshiriki, ambapo kila klabu itatakiwa kujitegemea kwa kila kitu iwapo kwenye kituo cha mashindano.
Hata hivyo, kwa klabu itakayothibitisha kushiriki lakini baadaye ikajiondoa baada ya ratiba kupangwa, itakabiliwa na adhabu ya kutoshiriki katika shughuli zinazoandaliwa na shirikisho kwa kipindi cha mwaka mmoja na pia adhabu nyingine itatolewa na Kamati ya Utendaji kadri itakavyoona.
Timu pia inatakiwa kufika kwenye kituo cha mashindano siku moja kabla ya kuanza kwa mashindano hayo na zile zitakazochelewa na kukuta michezo yake imepita zitahesabika zimeshindwa.
Kanuni imeeleza wazi kuhusu usajili wa wachezaji, ambapo ni lazima kujazwa kwa fomu maalumu za shirikisho hilo zitakazorudishwa kabla ya mashindano kuanza na kupewa leseni, ambapo ni wawe tu watumishi wa umma kutoka kwenye Wizara, Ofisi za Mikoa, Idara zinazojitegemea.
Wakala za Serikali; hata hivyo, klabu itakayochezesha wachezaji wasio watumishi wa umma na waliotoka kwenye mashirikisho mengine, yakiwemo Bamata, Shimuta na Shimisemita, itakabiliwa na adhabu ya faini ya Sh milioni 1 na kufutiwa michezo yote iliyosajili.
Kila klabu inatakiwa kulipa ada ya uanachama kiasi cha Sh 600,000 na ada ya ushiriki Sh 400,000 kabla ya kuanza kwa mashindano kwani zilizoshindwa hazitaruhusiwa kushiriki. Hata hivyo, ili kuondoa dhana ya kuchezesha wachezaji ambao sio watumishi wa umma, ni lazima kila mshiriki wa mashindano haya awe na kitambulisho cha kazi, salary slip ya karibuni na kadi ya Bima ya Afya.
Kwa upande wa waamuzi na makamisaa wa michezo yote itakayoshindaniwa watakapoboronga kwa kutoa maamuzi yenye utata na kushindwa kutafsiri vyema sheria za michezo husika, wataondolewa kwenye orodha na nafasi zao watapewa wengine baada ya vyama vya waamuzi wa michezo husika wa mkoa huo.
Kanuni pia zimeonesha timu shiriki zenye michezo kulingana na ratiba ya mashindano inatakiwa kufika uwanjani si chini ya dakika 45 kabla ya mchezo kuanza, hata hivyo timu itakayochelewa na kwenda kinyume na utaratibu huu itapewa adhabu ya faini itakayopangwa na kamati ya rufaa na nidhamu, pia kunyimwa ushindi endapo itashinda baada ya kukubaliwa kucheza mchezo husika.
Kila timu italazimika kuvaa sare (jezi) ya mchezo husika ambayo aliionesha kwenye mkutano wa maandalizi ya mchezo (pre-match meeting) unaofanyika saa chache kabla ya kuanza kwa mchezo husika, na endapo itavaa jezi tofauti itapewa adhabu; halikadhalika timu itahesabiwa kuwa na utovu wa nidhamu endapo itakataa kutoa mkono kwa mgeni rasmi itachukuliwa hatua za kinidhamu pamoja na kutozwa faini.
Hata hivyo, kanuni imewakumbusha viongozi wa klabu zote shiriki ni lazima kuhudhuria mikutano inayopangwa na Shirikisho au kamati mbalimbali kwa kipindi chote cha mashindano na kiongozi asiyehudhuria atapigwa faini na endapo atachelewa kufika kwenye mkutano atatozwa faini.
Kanuni imewakumbusha viongozi wa klabu shiriki kuwasilisha kwa maandishi malalamiko au rufaa kwa Katibu wa kamati ya nidhamu; na endapo timu haitaridhika na maamuzi yaliyotolewa na kamati hiyo wana nafasi ya kukata rufaa kwa maandishi kwenye Kamati ya Utendaji. Pia imeidhinishwa ni marufuku kupeleka masuala ya michezo hii mahakamani.
Waajiri wa timu ambazo zitajitoa bila kuwa na sababu za msingi wataandikiwa barua ya kuiondoa timu hiyo kwenye kituo cha mashindano na itapigwa faini kwa kuonesha utovu wa nidhamu, halikadhalika atapokea pia barua ya kuonesha nidhamu mbovu kwa timu yake endapo itasababisha kuvunjika kwa amani na mchezo na pia itapigwa faini na kupokwa ushindi endapo walikuwa wakiongoza hadi mchezo kuvunjika.
Timu zote zitakazochezesha wachezaji ambao si watumishi wa umma au wa wizara, taasisi yake maarufu kama mamluki itapigwa faini pamoja na kufungiwa kutoshiriki kwenye shughuli za Shimiwi kwa kipindi cha miaka mitatu (3) na mwajiri wake atawasilishiwa barua ya kumtaarifu juu ya suala hilo.
Hata hivyo, kanuni zimewataka wachezaji wa timu zote shiriki kuwemo wote kwa idadi yao kamili kama walivyokuja katika sherehe za ufunguaji wa michezo hii na Oktoba 15, 2022 siku ya ufungaji na endapo watakwenda kinyume watatozwa faini pamoja na mwajiri wake kupewa taarifa kwa njia ya barua.
Kwa kiasi kikubwa kanuni zimeainisha makosa mbalimbali, ikiwemo upangaji wa matokeo timu zilizohusika zitafutiwa matokeo na kuchukuliwa hatua za kinidhamu na kutozwa faini.