2024 Imetuachia haya katika burudani

MWAKA 2024 umeshuhudia matukio mengi makubwa katika tasnia ya burudani nchini Tanzania. Baadhi ya matukio haya yamevuta hisia za wengi na kuwa gumzo katika majukwa mbalimbali.
Leo tunakupitisha kwenye baadhi ya matukio hayo katika kuufunga mwaka 2024.
Mahusiano ya Marioo na Paula
Msanii wa Bongo fleva nchini Omary Mwanga ‘Marioo’ alipata mtoto na mchumba wake Paula baada ya kuwa kwenye mahusiano yaliyokuwa gumzo katika majukwa mbalimbali.
Marioo aliandaa mtukio mbalimbali ya kujipongeza na kumpongeza Paula kwa zawadi yam toto huyo aliyepewa jina Amara.
Alikiba kuzindua kituo cha Crown
Msanii wa Bongo fleva Ali Kiba mwaka 2024 aliamua kuingia mazima kwenye vyombo vya habari baada ya kuzindua Redio na Tv ya Crown Kiba anaungana na msanii Naseeb Abdul, Diamond ambaye naye kwa muda mrefu amewekeza kwenye vyombo vya habari kwa kuwa nai kituo cha Wasafi.

Uhusiano wa Hamisa Mobetto na Azizi Ki
Mwanamitindo na mjasiriamali Hamisa Mobetto alihusishwa na tetesi za kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mchezaji wa Yanga, Stephan Aziz Ki. Ukaribu wao ulionekana katika matukio mbalimbali, ikiwemo tuzo za wanamichezo bora na uzinduzi wa duka la Hamisa. Hata hivyo, suala hilo lilibaki kuwa tetesi bila uthibitisho rasmi.
Niffer na Diva kuchangisha pesa za Kariakoo
Jennifer Jovini maarufu kama Niffer alijikuta matatani baada ya agizo lililotolewa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuwa akamatwe kwa kosa la kuchangisha pesa za waliopata maafa ya Kariakoo kwa kinyume cha sheria bila kuwa na ruhusa kutoka kwenye kamati ya maafa Mtangazaji Diva pia alijikuta matatani.
Nandy kuzimia jukwaani
Msanii Nandy alizimia ghafla akiwa jukwaani katika tamasha la Marioo lililofanyika Warehouse Masaki. Sababu iliyotajwa ni uchovu uliotokana na ratiba ngumu ya kazi.
Ndoa ya Haji Manara na Zaylisa
Msemaji wa zamani wa Simba na Yanga Haji Manara hakuwa nyuma mwaka 2024 nae aliingia katika matukio yaliyotikisa mwaka 2024 katika uga wa burudani baada ya kumvalisha pete msanii wa filamu anayetamba kwenye tamthilia ya Jua Kali.
Marioo kukabiliwa na kesi ya madai
Msanii Marioo alikumbwa na kesi ya madai baada ya kushindwa kutumbuiza katika shindano la Mr & Miss Vyuo Vikuu Kanda ya Kaskazini lililoandaliwa na kampuni ya Kismaty. Kampuni hiyo ilidai imepata hasara ya Sh milioni 550 kutokana na kuvunjwa kwa makubaliano hivyo kudai fidia.
Tanzania Muziki Award gumzo!
Tuzo hizo zilizua maswali mengi baada ya mambo kwenda tofauti na mashabiki walivyotarajia hii ilitokana na msanii Faustina Mfinanga ‘Nandy’ na Zuhura Othuman ‘Zuchu’ kupewa tuzo ambazo wengi waliamini zinafanana jambo lilosababisha wengi kuhoji uhalali wa tuzo zenyewe.
Zuchu kurushiwa vitu jukwaani
Katika tamasha la Wasafi Festival lililofanyika jijini Mbeya, msanii Zuchu alilazimika kushuka jukwaani baada ya kurushiwa vitu na mashabiki, ikiwemo chupa za maji. Tukio hili liliibua mjadala kuhusu tabia za mashabiki katika matamasha.
Chid Benz kushushwa jukwaani
Msanii Chid Benz alishushwa jukwaani na walinzi katika tamasha la Best Vibes lililofanyika viwanja vya Posta Kijitonyama baada ya kupanda bila kuwa kwenye ratiba rasmi. Muonekano wake wa kuvaa yebo yebo pia ulizua mijadala mitandaoni.
Ali Kiba kuhamia Simba
Msanii wa Bongo fleva Ali Kiba alitoa kali ya mwaka baada ya kuamua kuvunja mapenzi yake na klabu ya Yanga na kutangaza kuhamia Simba. Ali Kiba alinukuliwa akisema kuwa moja ya sababu ya kumundoa Yanga ni kutothaminiwa na klabu hiyo licha ya mahaba yake kwao hivyo Simba wameiona thamani yake na ameamua kujiunga nao.
Tangu kujiunga na Simba Kiba amekuwa akihusishwa kwenye matukio mbalimbali ya timu hiyo ikiwemo nyimbo za hamasa na kutumbuiza kwenye matamasha yao.
Nay wa Mitego na BASATA
Msanii Nay wa Mitego aliitwa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) kwa kutoa wimbo wake “Nitasema” bila kibali. Wimbo huo ulidaiwa kuwa na maudhui ya uchochezi na kupotosha jamii.
Snura kuacha muziki
Mwaka 2024 msanii wa Bongo fleva Snura Mushi ‘Snura’ alitangaza kuacha kuimba nyimbo za bongo fleva na kumrudia Mungu wake na kuomba nyimbo zake zisipigwe sehemu yoyote.
Wadau mbalimbali walikuja na mitazamo tofauti lakini mwisho wa siku waliheshimu uamuzi wake.
Hayo ni miongoni mwa matukio yaliyotikisa katika sekta ya burudani kwa mwaka 2024. Nikutakie heri ya mwaka 2025.




