Mahusiano

Wasanii wanavyotumia mahusiano yao kama kiki

WASHKAJI wanaamua kukutana na kufanya sherehe ya pamoja baada ya kupotezana kwa takribani miaka kumi na tano tangu wamalize shule mwaka 2006.

Kama ilivyo kawaida mnapokutana watu mliosoma darasa moja, baada ya kitambo kirefu kupita, mambo huwa yamebadilika sana; huyu kanenepa kidogo, yule kawa handsome zaidi, hawa wana watoto, wale wajawazito n.k.

Kwa kifupi, kukutana kwenu kunaifanya siku hiyo kuwa tamu sana na ya kusisimua! Sasa shughuli hii isingekuwa shughuli kama mtu mmoja asingefika jioni hii; huyu anaitwa Eugene ila kwa sasa dunia inamfahamu kama Xavier.

Xavier ni staa wa muziki wa pop na mwigizaji wa filamu ambaye pia alimaliza shuleni hapo na ndiye aliyekuwa akisubiriwa kwa hamu kubwa na watu wengi ingawa wapo pia ambao hawataki hata kumwona.

Siku hii watu wanakula bata na kama haitoshi, Xavier anawaalika katika jumba lake la kifahari kwa ajili ya kwenda kufanya sherehe nyingine ‘after party’ ili kiu ya kutoonana miaka kumi na tano ikate kabisa.

Saa kadhaa baada ya sherehe hii kwenye jumba la Xavier, polisi wanapata taarifa kuwa kuna kitu kimetokea katika sherehe hiyo kiasi cha kukuta mwili wa mtu mmoja aliyekufa ukiwa kando ya jumba hilo la kifahari. Ni nani mtu huyu?

Hebu ngoja kwanza… mbona kama ni… dah, huyu ni Xavier ambaye ndiye aliwaalika wenzie nyumbani kwake kwa ajili ya after party! Sasa imekuwaje?

Uchunguzi wa awali wa polisi unaonesha kwamba mtu huyu hakuanguka wala kuteleza kwa bahati mbaya kutoka juu ya jumba lake la kifahari bali alisukumwa umbali mrefu toka juu ya jumba hilo na kufa papo hapo.

Na sasa habari kwenye vituo mbalimbali vya runinga zinajikita kumwonesha staa Xavier huku kifo chake kikiitikisa dunia kwa kuwa ndiyo kwanza ameanza kufanya vizuri na kuweka alama kwenye ulimwengu wa muziki na filamu.

Eti leo anatajwa kuwa amekufa kando ya jumba lake la kifahari dakika chache tu tangu awaalike wanafunzi wenzake wa zamani kuja kufanya party nyumbani kwake!

Sasa polisi wanaamua kuwaweka chini ya ulinzi mara moja watu wote waliokuwa na Xavier usiku huu nyumbani kwake ili kujua nani amehusika na mauaji haya ya kikatili na nini sababu ya mauaji haya. Sijui ni nani mhusika wa mauaji ya Xavier? Au ni bonge anayeitwa Aniq?

Huyu amekuja kwenye sherehe hii kwa sababu moja tu ya kumfuata Zoe, mwanamke ambaye alikuwa anamtesa miaka yote shuleni na hakuwahi kumpa moyo wake.

Miaka yote Aniq alishindwa kubanjuka na Zoe na leo wanapokutana baada ya miaka kumi na tano anapata nafasi ya kuwa karibu naye, lakini anashindwa kumpata kwa kuwa kizuizi kikubwa ni staa Xavier ambaye naye alikuwa anamtaka Zoe.

Mbaya zaidi leo Zoe anashoboka kwa Xavier kwa sababu ya ustaa wake na kumpuuza Aniq kitendo kinachomnyong’onyesha Aniq. Aniq anashuhudia akipokwa tonge mdomoni. Je, inawezekana Aniq ndiye muuaji? Sidhani! Sasa hapa muuaji ni nani? Au ni Brett?

Huyu ni miongoni mwa wanafunzi hawa wa zamani waliokuja kwenye party baada ya kupotezana kwa muda mrefu. Huyu mwamba pia alikuwa ana misheni yake moyoni, amekuja kumfuata mwanadada Zoe, mwanamke aliyekuwa na Aniq kisha akaondoka na Xavier.

Zoe ni mke wake ila kwa sasa wametengana, na wamebahatika kupata mtoto mmoja. Hadi sasa moyo wa Brett bado uko kwa Zoe na hapa amekuja kuhakikisha hakuna mwanamume yeyote atamuopoa Zoe.

Katika kufuatilia akamwona Zoe akiwa na Aniq lakini haikumshtua sana kwani anajua Aniq ni domo zege lakini kumwona staa Xavier ambaye walikuwa hawapatani tangu shule, eti ambebe mkewe! Kwake hiyo ni dharau kubwa.

Huenda labda hasira za kuchukuliwa mkewe ndizo zilimpeleka nyumbani kwa Xavier na kufanya mauaji hayo? Lakini… hebu ngoja kwanza! Mbona kama polisi wamekuta kitu fulani kwenye mwili wa Xavier! Wamekuta pombe ambayo mwanzo alionekana nayo bibie Chelsea.

Chelsea pia alikuja kwenye sherehe hii japo hakuwa na furaha kwa sababu kuna kitu kibaya alifanyiwa na Xavier miaka mingi iliyopita na ameishi na dukuduku miaka yote hadi leo ilipoandaliwa sherehe hii ya kuwakutanisha tena.

Isije kuwa amekuja hapa ili amghilibu Xavier aingie kwenye kumi na nane zake kisha amleweshe pombe na kumtoa uhai! Ila… mbona kama bado haiwezekani? Haiwezi kuwa kirahisi hivyo! Sasa ni nani amehusika na mauaji haya? Anaweza kuwa Yasper? Walt?Au Ned?

Maana hawezi kuwa Zoe kwani yeye alionesha kumzimikia Xavier na Xavier hakuwa na tatizo lolote na Zoe japo Brett alikuwa na tatizo na Xavier… The After Party ni moja ya series tamu sana kwenye runinga kwa sasa.

Hauhitaji kuwa na akili kubwa sana kuielewa tamthilia hii, ni simple lakini moja ya kazi bora sana mtandaoni kwa sasa. Ni kazi iliyotoka rasmi Januari 28, 2022.

Related Articles

Back to top button