Kunoga kuzichapa nchini Kazakhstan

BONDIA wa wa Ngumi za Kulipwa kutoka Tanzania, Jamal Kuninga, anatarajia kupanda ulingoni Jumapili, Februari 23, 2025, katika pambano dhidi ya mwenyeji wake, Samat Zhetibayev, nchini Kazakhstan.
Pambano hilo la uzani wa ‘Bantam’, lisilo la ubingwa, litafanyika kwa raundi sita katika ukumbi wa Halyk Arena Sport Complex, uliopo mji wa Aktau, nchini Kazakhstan.
Mara ya mwisho Kuninga kupanda ulingoni ilikuwa Oktoba 25, 2024, ambapo alimtandika bondia Elly Ally kwa ‘points’ za majaji wote watatu katika ukumbi wa Tanzanite, mkoani Morogoro.
Kuninga ni bondia namba saba nchini Tanzania kati ya mabondia 51, pia ni wa 209 kati ya mabondia 1,149 duniani. Ana hadhi ya nyota moja na nusu, akiwa ameshinda mapambano 9 kati ya 13, akishinda mawili kwa ‘KO’, akipoteza mawili, moja kwa ‘KO’, na kutoka sare mara mbili.
Mpinzani wake, Zhetibayev, ni bondia namba mbili kati ya mabondia watatu nchini Kazakhstan, na anashika nafasi ya 191 duniani. Pia ana hadhi ya nyota moja na nusu, akiwa ameshinda mapambano 6 kati ya 7, na 4 kati ya hayo kwa ‘KO’, akipoteza pambano moja.