Golf

Woods ajiondoa gofu kutafuta matibabu

FLORIDA, Marekani: Mchezaji wa Gofu wa kulipwa, Tiger Woods, ametangaza kujiondoa kwa muda kwenye mchezo huo ili kutafuta matibabu na kuangazia afya yake, kufuatia kukamatwa baada ya kuhusishwa na ajali ya gari iliyotokea Florida, Marekani.

Woods mwenye umri wa miaka 50, ambaye amewahi kutwaa mataji 15 ya mashindano makubwa ya gofu (majors), alikamatwa na kufunguliwa mashtaka ya kuendesha gari akiwa chini ya ushawishi wa kilevi au dawa za kulevya baada ya kugonga lori na gari lake kupinduka mwishoni mwa wiki.

Mbali na shtaka hilo, pia anakabiliwa na mashtaka ya kusababisha uharibifu wa mali pamoja na kukataa kufanyiwa kipimo halali kilichoombwa na mamlaka.

Kupitia taarifa yake aliyoiweka kwenye mtandao wa X, Woods amesema anatambua uzito wa hali inayomkabili kwa sasa na ameona ni muhimu kuchukua muda mbali na mchezo huo ili kujijenga upya kiafya.

“Ninaelewa kwa uzito mkubwa hali niliyojikuta nayo sasa. Najiondoa kwa muda ili kutafuta matibabu na kuzingatia afya yangu. Hii ni muhimu ili niweze kuweka mbele ustawi wangu na kujenga ahueni ya kudumu,” amesema Woods.

Kwa mujibu wa ripoti ya polisi iliyotolewa Jumanne, Woods alikutwa na vidonge viwili vya hydrocodone, dawa inayotumika kupunguza maumivu makali, huku maofisa wakieleza kuwa alikuwa akionekana mchovu, mwenye mwendo wa polepole, akitokwa jasho jingi.

Kupitia mawakili wake, Woods tayari amewasilisha utetezi wa maandishi mahakamani akikanusha makosa yote yanayomkabili.

Kabla ya tukio hilo, Woods alikuwa hajafunga kabisa mlango wa kushiriki mashindano ya Masters yanayotarajiwa kufanyika mwezi ujao, licha ya kutocheza mashindano makubwa tangu aliposhindwa kufuzu hatua inayofuata kwenye The Open mwaka 2024.

Related Articles

Back to top button