William Saliba apania Kombe la Dunia
						NYOTA wa Arsenal William Saliba ambaye kwa sasa ana kiwango bora Ligi Kuu Uingereza amesema ni ndoto yake kuanza kikosi cha kwanza cha Ufaransa kwenye michuano ya Kombe la Dunia.
Miaka mitatu baada ya uhamisho wake kutoka St Etienne kwa pauni milioni 25 sawa na shilingi bilioni 65.9 hatimaye beki huyo wa kati ameingia kikosi cha kwanza akianza michezo saba ya Arsenal ya Ligi Kuu msimu huu akifunga mabao 2.
“Ndoto yangu ni kucheza Kombe la Dunia nikiwa na nchi yangu na ninatumaini nitakuwa kwenye timu kwa ajili ya Kombe la Dunia,” amesema Saliba.
Washindani wa Saliba kwenye nafasi ya beki wa kati katika kikosi cha Ufaransa ni pamoja na beki wa Manchester United Raphael Varane, Jules Kounde wa Barcelona, Dayot Upamecano wa Bayern Munich na Benoit Badiashile wa Monaco.
Michuano ya Kombe la Dunia imepangwa kuanza Novemba 20 hadi Desemba 18, 2022 nchini Qatar.
				
					



