Wenye ulemavu kuogelea wanahitaji msaada milioni 15.6

DAR ES SALAAM: CHAMA cha Kuogelea kwa Watu Wenye Ulemavu Tanzania (TPSA) kimeomba wadau wa michezo, makampuni, taasisi, na watu binafsi kutoa msaada wa kifedha au vifaa ili kufanikisha mashindano yake ya Tatu ya Taifa ya Utambuzi wa Vipaji.
Kiasi ambacho inahitaji kwa ajili ya mashindano hayo ni sh milioni 15.65. Mashindano hayo yatafanyika Oktoba 11, 2025, katika bwawa la kuogelea la Shule ya Sekondari ya Shaaban Robert, Upanga, Dar es Salaam.
Mashindano haya yanalenga kutambua vipaji vipya vya waogeleaji wenye ulemavu wa viungo, macho na akili, na ulemavu wa aina mbalimbali.
Zaidi ya hayo, yatasaidia kuendeleza ujuzi wa waogeleaji, kuhamasisha ushiriki, na kujenga timu ya taifa itakayoshiriki mashindano ya kimataifa, ikiwemo michezo ya Paralympic itakayofanyika Los Angeles 2028.
Ramadhan Namkoveka, Katibu Mkuu wa TPSA, amesema, “Tunawaalika wadau wote kujitokeza kusaidia kifedha au vifaa. Mchango wowote utasaidia kuboresha mashindano na kuendeleza mchezo wa kuogelea kwa watu wenye ulemavu nchini,”
Aidha, TPSA inatoa wito kwa waogeleaji wote kutoka kote nchini, wakiwemo wale walio nje ya Dar es Salaam, kujiandikisha kushiriki. Dirisha la kujiandikisha linafunguliwa hadi Septemba 29, 2025.
Mashindano haya ni fursa ya kipekee kwa waogeleaji kuonyesha vipaji vyao, kujenga timu ya taifa, na kuwakilisha Tanzania kwenye mashindano makubwa ya kimataifa.