Wavu Zanzibar kuanza Septemba 1

LIGI Kuu ya Zanzibar ya mpira wa wavu inatarajiwa kuanza rasmi Septemba mosi
mwaka huu.
Ligi hiyo ambayo itashirikisha timu 10 zikiwemo tano za wanawake na tano za wanaume, itachezwa katika viwanja vya Mafunzo na cha Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU).
Kwa mujibu wa ratiba ya ligi hiyo iliyotolewa na Kamati ya Mashindano ya Chama cha Mpira wa Wavu Zanzibar (ZAVA), ligi hiyo itamalizika Septemba 13 mwaka huu.
Timu zinazoshiriki ligi hiyo kwa wanawake ni JKU, KMKM, KVZ, Chuoni na Mafunzo na kwa wanaume ni ni KVZ, Nyuki, Mafunzo, JKU na Chuoni.
Aidha, ratiba hiyo inaonesha kwamba kila siku kutakuwa na michezo miwili, ambapo siku ya kwanza wakati wa saa 2:00 za asubuhi katika Uwanja wa Mafunzo, KMKM wanawake itacheza na KVZ na saa 10:00 jioni, KVZ itacheza dhidi ya JKU wanaume.
Hata hivyo, Mafunzo na Nyuki zinatarajia kucheza siku inayofuata kuanzia saa 2:00 asubuhi uwanjani hapo kabla ya saa 10:00 jioni, JKU itaumana na Chuoni mechi zote za wanaume.