Waogeleaji wanne kwenda Romania

DAR ES SALAAM: WAOGELEAJI wanne wa timu ya taifa ya kuogelea wanatarajiwa kuondoka nchini kuelekea Romania kwa ajili ya kushiriki Mashindano ya Dunia ya Vijana yatakayofanyika kuanzia Agosti 18 hadi 25, 2025.
Wachezaji watakaoiwakilisha Tanzania ni Philbertha Demelo, Romeo Mwaipasi, Austin Okoren, na Bridget Heep. Kwa mujibu wa taarifa rasmi kutoka kwa Baraza la Michezo la Taifa, maandalizi yote muhimu yamekamilika, na timu hiyo inatarajiwa kuondoka Jumamosi kesho.
Mkurugenzi wa Ufundi wa Chama cha Kuogelea Tanzania (TSA), Amina Mfaume, amesema timu iko katika hali nzuri na tayari kuonesha uwezo wao katika medani ya kimataifa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TSA, David Mwasyoge, alieleza kuwa mashindano hayo ni sehemu ya mpango mkubwa wa kuendeleza waogeleaji vijana wa Tanzania, hasa wenye umri wa miaka 14 hadi 18.
Amesema kuwa kundi hili lina umuhimu mkubwa katika mustakabali wa taifa kwenye michezo, na ndilo linalobeba matumaini ya ushindani wa baadaye katika anga za kimataifa.
Mwasyoge amesisitiza nafasi ya serikali, wadau na wazazi katika kuhakikisha kuwa vijana hao wanapata mazingira bora ya maandalizi.
Ofisa Michezo wa Baraza la Michezo la Taifa BMT Charles Maguzu alitoa pongezi kwa Rais Samia Suluhu Hassan, kwa mchango wake mkubwa katika maendeleo ya michezo.
Amesema serikali kupitia sera na hatua madhubuti, imefanikisha upatikanaji wa posho kwa wachezaji na kuweka mazingira bora ya usafiri na maandalizi.
Maguzu, aliongeza kuwa ushiriki wa wachezaji hao kimataifa utawasaidia wachezaji sio tu kujenga uzoefu, bali pia kujenga heshima ya taifa kimataifa na kuahidi kuwa serikali itaendelea kushirikiana na vyama vya michezo nchini kwa lengo la kukuza sekta hiyo.