Vilemba, Kofia zimerahisisha mambo!

KATIKA ulimwengu wa mitindo kila siku wabunifu huumiza vichwa kuja na mitindo mbalimbali mipya kwa lengo la kubadili mionekano ya watu na kuwafanya kuwa kivutio kwenye majukwaa wanayopanda.
LEO tutaongelea jinsi vilemba na kofia vinavyoweza kukufanya uonekane nadhifu na mwanamitindo wa kisasa. Awali ufungaji wa vilemba ulionekana zaidi misibani, makanisani na mashambani lakini sasa hali imebadilika.
Unaweza kufunga kilemba ukaenda sehemu yoyote ile ya heshima hata kwenye mikutano mikubwa na ukaonekana nadhifu.Kufunga kilemba kwenye shughuli mbalimbali kulitokana na wenzetu wa nchini Nigeria na Congo walivyoamua kuendeleza utamaduni wao huo na kila kukicha kubuni mitindo mipya ya ufungaji wa vilemba.
Siyo wote tuna utaalamu wa kufunga kilemba licha ya kuwa tunapenda mtindo huo, ufungaji wa kilemba unahitaji mtu mwenye ustadi wa kufanya kazi hiyo ili kuendana na mitindo mbalimbali iliyopo.
Wabunifu wa mitindo walienda mbali zaidi na kutengeneza kofia za staili mbalimbali ambazo zinafanana na vilemba. Ukiangalia kwa haraka unaweza usitambue kama aliye mbele yako amefunga kilemba au amevaa kofia, hilo linatokana namna zilivyotengenezwa kisasa.
Kofia hizi zipo katika mitindo na rangi tofauti tofauti, na huvaliwa na kumpa fursa mtu kuchagua kulingana na matakwa yake.Uzuri wa kofia hizi zinaweza kuvaliwa mahali popote na mvaaji akaendelea kuonekana wa kisasa tofauti na ilivyokuwa awali.
Ilikuwa nadra sana kumkuta mtu kavaa suti na kofia. Hali imebadilika mtindo huu wa kofia unaruhusu kupangilia vazi lako la suti na kuendelea kuonekana nadhifu.
Unaweza pia kuvaa suruali yako ya kitambaa, jeans na blauzi utakayopenda kisha juu ukapiga kofia kulingana na rangi uliyochagua.
Ukivaa nguo ya kitenge ndio mahala pake zinaendana sana na kofia au nguo ya rangi moja ukichanganya na kofia ya kitenge inanoga sana. Ingawa kila mtu ana chaguo lake ila ukitaka kunoga zaidi ukivaa kofia hii uvae kiatu chenye kisigino kirefu kinakuongezea unadhifu katika mapigo yako.
Juma lijalo tutaangazia mtindo mwingine utakaokufanya uende sambamba na mitindo inayotamba ulimwenguni katika mikato yako.