UNI challenge yaibuka kidedea

MECHI ya kirafiki iliyochezwa hivi karibuni kati ya Timu ya Guardian of the Peak na Uni Challenge imehitimishwa kwa timu ya Uni Challenge kutoka kifua mbele, ambapo timu hiyo ilijinyakulia Kombe la Guardian of the Peak Season Two, baada ya ushindi wa mikwaju ya penalti.
Katika dakika 90 za mchezo huo, timu hizo zilitoshana nguvu kwa kufungana mabao 4–4, hali iliyolazimu kuamuliwa kwa mikwaju ya penalti ambapo Uni Challenge Team iliibuka na ushindi wa mabao 2–0 dhidi ya Guardian of the Peak Team.
Akizungumza na Spoti leo baada ya mchezo huo, Ram Ally, Mkurugenzi wa Ram Film Company ambao ndio waandaaji wa mradi wa Guardians of the peak, amesema kuwa lengo la mechi hiyo ni kuwakutanisha vijana, kuimarisha mshikamano, pamoja na kuwahamasisha kuachana na makundi hatarishi yanayoweza kuhatarisha maisha yao na mustakabali wa jamii.
Ameongeza kuwa mechi hiyo pia imelenga kuendelea kuwaunga mkono vijana katika jitihada za utunzaji wa mazingira, hususan matumizi ya Nishati safi na salama, sambamba na kampeni za kulinda vivutio vya asili ikiwemo Mlima Kilimanjaro.
Mechi hiyo imeelezwa kuwa ni sehemu ya mpango endelevu wa kutumia michezo kama chombo cha kuleta mabadiliko chanya kwa jamii, hasa kwa vijana nchini.




