Kikapu

TWBA yaita wadau kwenye mafunzo ya kikapu

CHAMA cha Kikapu kwa watu wenye ulemavu (TWBA) kimehimiza wadau mbalimbali hususan wenye ulemavu na wasio na ulemavu kujitokeza na kushiriki mafunzo maalum ya mchezo huo.

Kwa mujibu wa taarifa ya Katibu Mkuu wa TWBA Abdallah Mpogole, mafunzo hayo yatalenga maeneo mawili ukufunzi katika mchezo lakini pia eneo la Uamuzi na yatakuwa ya kinadharia na vitendo.

Amesema mpira wa kikapu kwa watu wenye ulemavu ni mchezo wenye hadhi ya Paralimpiki yaani Olimpiki maalumu ya wachezaji wa mchezo huu kwa watu wenye ulemavu wa eneo la chini la kiwiliwili kwa ulemavu utokanao na athari za polio, matatizo ya ukuaji finyu wa mifupa hali kadhalika ulemavu wa kupoteza viungo kutokana na ajali mbalimbali.

“Kama Chama cha Mpira wa Kikapu tumeona ni wakati muafaka kuendesha mafunzo haya kwa jamii nzima ya wanamichezo, waalimu wa shule za msingi na sekondari, waalimu wa shule maalumu za watu wenye ulemavu,taasisi mbalimbali zinazosaidia vituo vya watu wenye ulemavu na watanzania kwa ujumla ili kupata maarifa ya awali ya mchezo kuupeleka mbele kifursa na kuleta tija,” Amesema.

Amesema kozi au mafunzo haya maalumu ya awali yatachukua siku tano kuanzia Mei13 hadi 17 mwaka huu katika Viwanja vya JMK Park Kidongo chekundu Dar es salaam.

Mpogole amesema mafunzo hayo yataongozwa na mkufunzi wa kitaifa mwenye ujuzi wa mchezo wa Mpira wa Kikapu kwa watu wenye Ulemavu Robert Manyerere akishirikiana na Shabani Mahobonya ambaye ni Mwamuzi wa kimataifa wa mchezo huu duniani wakishirikiana na baadhi ya makocha na waamuzi wa mchezo huo.

“Gharama za ushiriki wa kozi hii ya awali ni fedha tasilimu Elfu Arobaini (40,000)
ambazo zitakuwa ni malipo ya wakufunzi, washiriki kupata vifaa vya kupatia mafunzo kadhalika kuwezesha kupata cheti cha awali kuthibitisha ushiriki wa mafunzo pia maboresho mengine yenye tija kwa washiriki..

“Fedha kwa ajili ya ushiriki wa mafunzo zitalipwa M Pesa Lipa Nambari : 5272793 Tanzania Wheelchair Basketball Association au Benki ( TCB)
Tanzania Commercial Bank akaunti namba 110218000478 Tanzania Wheelchair Basketball Association,” amesisitiza

Related Articles

Back to top button