La Liga

Timu ya Ronaldo yashuka daraja LaLiga

SEVILLE:REAL Valladolid, timu inayoshiriki ligi kuu ya nchini Spain Laliga ambayo Ronaldo De Lima ni mmiliki mkubwa zaidi wa hisa imeshuka daraja baada ya kipigo cha mabao 5-1 kutoka kwa Real Betis katika mchezo wa ligi kuu ya Spain Laliga wa jana Alhamisi usiku.

Valladolid waliopanda daraja mwaka jana wapo nafasi ya mwisho kwenye msimamo wa ligi baada ya kuvuna pointi 16 pekee katika michezo 33 waliocheza mpaka sasa wakishinda michezo minne pekee na mchezo mmoja tangu mapema Januari.

Akizungumza baada ya mchezo huo kocha mkuu wa kikosi hicho Alvaro Rubio ameiambia DAZN kuwa inasikitisha sana lakini wamestahili kushuka daraja baada ya mwendo mbaya uliowanyima nguvu ya kumudu mikiki mikiki ya Laliga.

“Ni siku ngumu sana kwetu, hali ya masikitiko imekikumba chumba chetu cha kubadilishia nguo lakini hatuna wa kumlaumu kwakuwa tumestahili hiki tulichopata tumevaa nembo hii na tumeshindwa kuiheshimu” amesema

Valladolid ilitegemewa kufanya makubwa hasa baada ya Ronaldo kuwa na hisa nyingi klabuni hapo akitarajiwa kufanya mabadiliko makubwa klabuni hapo na pengine icheze Ligi ya Mabingwa barani Ulaya msimu ujao lakini mambo ni tofauti na watalazimika kuanza upya huko Laliga 2.

Related Articles

Back to top button