Tetesi

Ten Hag: Xhaka bado ni muhimu sana kwetu

LEVERKUSEN: Meneja wa Bayer Leverkusen Erik ten Hag amesema kiungo wa klabu hiyo Granit Xhaka ni mchezaji muhimu sana kikosini hapo na timu hiyo ya Bundesliga haiwezi kumuacha raia huyo wa Uswizi aondoke kufuatia kuwepo ripoti zinazomhusisha na kuhamia ligi kuu ya England katika klabu ya Sunderland.

Leverkusen tayari imempoteza mchezaji wao muhimu Florian Wirtz na beki Jeremie Frimpong waliotimkia kwa mabingwa wa Premier League Liverpool huku beki wa kati Jonathan Tah akihamia Bayern Munich.

Mchezaji huyo wa zamani wa Arsenal Xhaka amehusishwa na kuhamia Sunderland huku wakala wake akiviambia vyombo vya habari vya Ujerumani kuwa nahodha huyo wa Uswizi mwenye umri wa miaka 32 ana makubaliano ya awali na klabu hiyo mpya iliyopanda daraja hadi Ligi Kuu ya England.

“Wakala anaweza kusema lolote. Lakini klabu hii tayari imepoteza wachezaji watatu muhimu. Hatutawaacha wachezaji wengine waende, hilo haliwezekani. Hilo litavuruga muundo na utamaduni wa kikosi chetu. Ni wazi, Granit ni kiongozi amesaini hapa kwa miaka mitano na amebakiza miaka mitatu kwenye mkataba wake. Ni muhimu sana kwetu hatutamwachia.” – Ten Hag ameviambia vyombo vya habari vya Ujerumani.

Xhaka aliisaidia Leverkusen kutwaa makombe mawili msimu wa 2023/24 waliponyanyua taji lao la kwanza la Bundesliga bila kupoteza mchezo wowote wakashinda pia Kombe la Ujerumani na kutinga fainali ya Europa League. Ameichezea Leverkusen mechi 99, akifunga mabao sita na asisti tisa.

Related Articles

Back to top button