Tamthilia ‘Nice to meet you’ yagusa nyoyo za watu

DAR ES SALAAM:WANAWAKE wengi wameeleza kupata faraja na hata kubarikiwa kupitia uigizaji wa msanii Hemed Suleiman ‘Hemed PHD’, anayejulikana kama Mchungaji Simon katika tamthilia maarufu ya Nice to Meet You.
Akizungumza na SpotiLeo wakati wa uzinduzi wa msimu wa pili wa tamthilia hiyo, Hemed alisema kumekuwa na mrejesho mkubwa kutoka kwa mashabiki, hasa wanawake waliowahi kupitia changamoto zinazofanana na wahusika wa tamthilia hiyo.
Katika msimu wa kwanza, Hemed aliigiza kama Simon, kijana mlokole aliyemsaidia mwanamke aliyejipatia kipato kupitia biashara ya kujiuza na kumrejesha katika njia ya imani. Swali linalobaki kwa mashabiki ni iwapo Simon ataendelea kushikilia ulokole au kurudi katika mapenzi ya zamani alipokuwa mwanafunzi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mahudhui na Masoko wa Startimes, David Malisa, amesema:“Hii ni sehemu ya kusapoti kazi za wasanii wa nyumbani na kuhakikisha jamii inapata maudhui bora yenye kuelimisha na kuburudisha.”
Tamthilia ya Nice to Meet You – Msimu wa Pili itaanza kurushwa rasmi Septemba 15, 2025 kupitia chaneli ya ST Swahili kwa kifurushi cha Nyota, kwa bei nafuu.
Aidha, msanii Lulu Abbas ‘Lulu Diva’, anayeigiza kama Brenda, amesema: kupitia tamthilia hii Nimepata tuzo ya msanii Bora wa kike mwaka 2025.
“Maisha ninayoigiza yananiumiza hata mimi mwenyewe, kwa sababu yamebeba uhalisia wa maisha ya mabinti wengi.”
Katika msimu wa kwanza, Brenda alikubali kuokoka, lakini msimu wa pili utabeba kiza au mwanga mpya? Swali hili linawaacha watazamaji na hamu kubwa.
Naye Linda Francis, anayeigiza kama Jemima, alisema msimu huu utaendelea kufichua namna wanawake wengi wanavyosukumwa kwenye maisha magumu na biashara ya kujiuza kwa kutafuta mali. “Msimu wa pili utakuwa wa kusisimua zaidi kwa sababu unaonyesha maamuzi magumu ya maisha,” amesema.
Tamthilia hii inabeba migogoro ya kifamilia, mapenzi, maumivu na changamoto zinazowakabili vijana wa sasa, huku ikilenga kuelimisha jamii kwa njia ya maigizo.