Africa

Taifa Stars, Bafana Bafana kumenyana leo

AFRIKA KUSINI: TIMU ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, ipo tayari kuivaa Afrika Kusini (Bafana Bafana) katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki utakaopigwa leo, huku Kocha Mkuu Hemed Morocco akithibitisha kuwa maandalizi yamekamilika na kikosi kiko imara kwa pambano hilo.

Akizungumzia mchezo huo, Kocha Morocco amesema, “Tuko vizuri na tayari kwa ajili ya mechi. Maandalizi yamekuwa mazuri na wachezaji wanaonesha kile tunachotaka kutoka kwao. Tumeweza kuizoea hali ya hewa vizuri, jambo ambalo ni muhimu kabla ya mchezo.”

Naye nahodha msaidizi wa Taifa Stars, Saimon Msuva, amesisitiza dhamira ya wachezaji kupigania taifa, licha ya changamoto ya kukutana na timu bora barani Afrika.

“Sio mchezo mwepesi ila tunahitaji kushinda. Tupo hapa kwa ajili ya nchi, tutapambania nchi kwa nguvu zote,” alisema Msuva.

Kwa upande wake mchezaji Seleman Gomez amesema endapo atapata nafasi ya kucheza ataonesha kile ambacho kimemfanya aitwe.

Katika viwango vya ubora vilivyotolewa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), mwezi Aprili vinaonesha Afrika Kusini inashikilia nafasi ya 56 duniani, huku Tanzania ikishika nafasi ya 107. Hata hivyo, historia inaonesha kuwa kila upande umewahi kupata ushindi katika mechi za nyuma.

Mwaka 2011, Tanzania ilipoteza kwa bao 1-0 dhidi ya Afrika Kusini kwenye mechi ya kirafiki, lakini Stars walirejesha heshima kwenye michuano ya COSAFA kwa kuibuka na ushindi wa bao 1-0.

Mashabiki wa soka wanatazamia mtanange wenye ushindani mkubwa, huku Taifa Stars ikisaka ushindi ambao utakuwa chachu kuelekea michezo ijayo ya kimataifa.

Related Articles

Back to top button