Soka La Ufukweni

Soka la Ufukweni yajipanga CECAFA

DAR ES SALAAM: KOCHA wa timu ya taifa ya soka la ufukweni, Jaruph Rajabu, amesema maandalizi kuelekea mashindano ya Baraza la Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) yanaendelea vizuri huku kikosi chake kikiwa katika hali nzuri ya kiafya na kiakili.

Mashindano hayo yanatarajiwa kufanyika kuanzia Julai 7, 2025, katika jiji la Mombasa, Kenya, yakishirikisha timu saba, zikiwemo Tanzania, Zanzibar, Uganda, Kenya, Burundi, pamoja na wageni kutoka Malawi na Visiwa vya Shelisheli.

“Tunashukuru hali za wachezaji ni nzuri. Tuna nafasi ya kwenda kuonesha ubora wetu ambao tumejiandaa nao kwa muda mrefu,” alisema Kocha Rajabu wakati akizungumza na wanahabari kuhusu maandalizi ya kikosi hicho.

Ameeleza kuwa mbali na mazoezi ya kawaida, timu inacheza michezo ya kirafiki kwa lengo la kuboresha mbinu za kiuchezaji na kuongeza kujiamini kwa wachezaji.

“Katika maandalizi yetu tunacheza michezo ya kirafiki. Yote haya ni kuendelea kuboresha maandalizi na kuwapa wachezaji nafasi ya kujiamini,” aliongeza kocha huyo.

Kocha Rajabu pia ametoa wito kwa Watanzania kuendelea kuzisapoti timu zote za taifa na kushikamana ili kuhakikisha zinapata matokeo chanya kwenye mashindano ya kimataifa.

Mashindano ya CECAFA kwa upande wa soka la ufukweni yanatarajiwa kuwa jukwaa muhimu la kuonesha vipaji vya wachezaji wa Afrika Mashariki na Kati, huku Tanzania ikitarajiwa kupeperusha vyema bendera ya taifa.

 

Related Articles

Back to top button