Ligi Kuu

Singida wakubali mziki wa Prisons

DODOMA: Meneja wa Singida Black Stars, Othmen Najjar amesema anashukuru kwa timu yake kupata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Tanzania Prisons, akieleza kuwa haikuwa mechi rahisi kutokana na ushindani mkubwa walioupata uwanjani.

Akizungumza baada ya mchezo huo jana kocha huyo amesema walikuwa wanatarajia upinzani mkali kutoka kwa Tanzania Prisons, hasa kutokana na uwezo wao wa kushambulia kwa kasi baada ya kupora mpira katikati ya uwanja.

“Tunamshukuru Mungu tumepata pointi tatu, haikuwa rahisi. Tulijua tutacheza dhidi ya timu imara ambayo ilituweka kwenye wakati mgumu, hasa walipokuwa wanapata mpira na kufanya mashambulizi ya haraka,” amesema.

Alikiri kuwa makosa ya mapema yaliwapa presha, akirejea bao waliloruhusu katika dakika za mwanzo, lakini aliipongeza timu yake kwa kuonesha mwitikio wa haraka na kusawazisha ndani ya muda mfupi.

Kocha huyo pia alizungumzia changamoto ya ubora wa uwanja, akisema uliathiri mfumo wao wa kawaida wa kucheza pasi fupi na kujenga mashambulizi taratibu kutoka nyuma.

Pamoja na changamoto hizo, alisifu juhudi za wachezaji wake kwa kupambana hadi mwisho na kuonesha nidhamu ya hali ya juu, huku akiahidi kuendelea kufanyia kazi mapungufu yaliyopo.

Akizungumzia ratiba ngumu waliyoipitia, kocha huyo amesema tangu ajiunge na timu hiyo Januari 4, kikosi kimepata mapumziko ya siku nne tu, huku pia kikikumbwa na kuondoka kwa wachezaji sita, hali iliyohitaji muda kujenga upya muunganiko wa timu.

Related Articles

Back to top button