Nyumbani

Singida Black Stars yaishika Yanga kooni

SINGIDA: UONGOZI wa Singida Black Stars umelalamikia kitendo cha Yanga SC kumchukua kocha wao, Hamid Miloud, bila kufuata taratibu za kisheria za taasisi.

Yanga SC ilimtangaza Miloud kuwa kocha mkuu wa timu hiyo, akichukua nafasi ya Sead Ramovic, ambaye ameondoka rasmi baada ya kuhudumu kwa miezi michache tu toka achukue nafasi ya Miguel Gamondi.

Ofisa Habari wa Singida Black Stars, Hussein Massanza, amesema kuwa kitendo cha Yanga kumtangaza Miloud bila mazungumzo yoyote na uongozi wa Singida ni cha hovyo na hakiendani na misingi ya uendeshaji wa taasisi za mpira wa miguu.

“Taarifa ya kocha wetu tuliona tu mitandaoni, jambo ambalo limetusikitisha sana. Hatukushirikishwa wala kuwa na majadiliano yoyote kabla ya uamuzi huo kufanyika. Tunaomba mashabiki wa Singida wawe watulivu, kwani idara yetu ya sheria inafuatilia suala hili ili kuona hatua za kuchukua kisheria,” amesema Massanza.

Ameongeza kuwa klabu haitachukulia suala hilo kwa mtazamo wa kishabiki bali wa kisheria, kwani linakiuka misingi ya taasisi yao na taratibu za kimkataba kati ya klabu na wafanyakazi wake.

“Tunaendesha klabu kwa misingi ya kisheria, na kila mfanyakazi ana mkataba rasmi. Inapotokea taasisi nyingine inavamia na kufanya maamuzi bila kufuata utaratibu, tunapaswa kujiuliza wanapataje usajili huo. Kwa kweli, tumesikitishwa sana na jambo hili,” alisisitiza Massanza.

Related Articles

Back to top button