Simba wala haina presha ikiivaa Petro Atletico kesho

LUANDA- NAHODHA wa Simba SC, Shomari Kapombe, amesema wanataka kuutumia mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Petro Atletico kama sehemu ya maandalizi ya mechi zijazo za Ligi Kuu na Mashindano mengine.
Mchezo huo unatarajiwa kuchezwa kesho Jumamosi nchini Angola ambapo tayari wekundu ni kama wamepoteza matumaini ya kusonga mbele kutokana na Mwenendo wa matokeo yaliyopita.
Kapombe amesema wachezaji wote wako tayari kwa ajili ya mchezo huo wa tano. Simba wanashika mkia kwa pointi moja pekee walizovuna katika michezo minne iliyopita.
“Tunaomba Watanzania wasiangalie matokeo yaliyopita, bali tuangalie jinsi tunavyoweza kufanya vizuri katika mchezo huu ambao tunautumia kama sehemu ya maandalizi kwa ajili ya mechi za Ligi Kuu,”amesema huku akiomba Watanzania waendelee kuwaombea dua.
Kapombe amesema kuwa kila mchezaji amejiandaa kikamilifu, na timu inakusudia kutoa kiwango bora katika mchezo huo.




