Nyumbani

Simba kuzindua jezi kishua

DAR ES SALAAM: KLABU ya Simba imetangaza kuzindua jezi zake mpya za msimu wa 2025/26 Agosti 27, 2025.

Msemaji wa Simba Ahmed Ally, amesema Dar es Salaam leo kuwa uzinduzi huo utafanyika kwa mtindo wa kipekee tofauti na miaka mingine wanavyofanya kwenye Ukumbi wa Super Dome, Masaki, Dar es Salaam.

Amesema safari hii uzinduzi wa jezi hizo umepewa hadhi ya kipekee kutokana na mdhamini mpya wa jezi, kampuni ya JayRutty Investment East Africa Ltd ikishirikiana na kampuni ya kimatifa ya Diadora.

“Tumeamua kufanya kitu kipya chenye mvuto kwa jamii na biashara ya jezi. Safari hii tutazindua kwa mtindo wa kipekee wenye hadhi ya ushua, utakaokutanisha wadau wakubwa wa Simba na mashabiki wanaotaka kununua jezi mara baada ya kuzinduliwa,” amesema Ally.

Katika uzinduzi huo, mashabiki watakaohudhuria watalipa Sh 250,000 na kisha watapewa jezi tatu za msimu mpya papo hapo ukumbini, huku wakipata burudani ya wasanii mbalimbali, muziki wa ‘live band’, vinywaji na chakula. Pia, kutakuwepo na mgeni rasmi ambaye ni gwiji wa soka barani Afrika atakayezindua rasmi jezi hizo.

Ahmed alifafanua kuwa jezi hizo hazitauzwa ukumbini, bali zitapatikana kwenye maduka yote yaliyo tayari kwa mauzo kuanzia usiku huo huo wa uzinduzi.

“JayRutty ameleta jezi nyingi sana, zinamtosha kila Mtanzania awe Simba au la. Bei ya jezi itakuwa Sh 45,000 na tayari oda imeanza kuchukuliwa rasmi na JayRutty pekee,” alisisitiza.

Katika usiku huo wa uzinduzi, washiriki pia watapata fursa ya kusikia historia ya Simba mwaka 1979 kupitia gwiji wa habari, Tido Mhando, kuhusu mchezo wa kihistoria wa klabu hiyo dhidi ya Mufulira Wanderers ya Zambia.

Related Articles

Back to top button