Nyumbani

Simba hii itacheza fainali kila mwaka- Ahmed

DAR ES SALAAM: MENEJA wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Klabu ya Simba, Ahmed Ally, amesema hatua ya timu hiyo kufuzu kucheza fainali ya mashindano ya Afrika ni mwanzo wa zama mpya kwa Wekundu wa Msimbazi.

Ahmed, amesema  sasa ni muda wa Simba SC kuwa mgeni wa kudumu katika hatua ya mwisho ya michuano hiyo kila msimu.

Akizungumza kuelekea fainali inayotarajiwa kuchezwa Jumapili, Mei 25 dhidi ya RS Berkane, Ahmed amesema kuwa baada ya ladha ya kufuzu fainali kwa mara ya pili tangu mwaka 1993, klabu hiyo haina mpango wa kurudi nyuma tena.

“Mwaka huu tumeingia fainali na haitajirudia tena kama ilivyokuwa mwaka 1993 ambapo ilituchukua zaidi ya miaka 30 kurudia hatua hii. Hii fainali ni sehemu ya maandalizi ya kushiriki fainali kwa misimu mingine inayokuja,” amesema.

Ahmed ameongeza  kuwa kuna watu ambao bado hawajamuelewa anaposema Simba itaendelea kuwa miongoni mwa timu kubwa barani Afrika, lakini amesisitiza kuwa mafanikio haya hayakuja kwa bahati, bali ni matokeo ya safari ya muda mrefu ya kushiriki robo fainali na hatua nyingine za juu.

“Tumetinga fainali, hatuwezi tena kusubiri miongo kupita. Mei 25 tunaenda kuwashangaza watu kwa kuifunga RS Berkane na kutwaa kombe. Ushindi huu utakuwa msingi wa mafanikio ya misimu ijayo,” amesema Ahmed.

Simba  sasa inasubiri kwa hamu kuchuana na RS Berkane huku mashabiki wao wakiwa na matumaini makubwa ya kuona historia ikiandikwa upya kwa klabu hiyo ya Tanzania.

Related Articles

Back to top button