Shah Rukh Khan atangaza kuacha kuvuta sigara

MUMBAI: NYOTA wa filamu za Bollywood, Shah Rukh Khan amewatangazia mashabiki wake kwamba zawadi yake kubwa siku yake ya kuzaliwa ni kuacha uvutaji wa sigara ambayo ni starehe yake ya muda mrefu.
Shah Rukh Khan amesema hayo wakati wa hafla yake alipokutana na mashabiki zake aliposherehekea kuzaliwa kwake akitimiza miaka 59, ambapo amewahakikishia mashabiki hao kwamba ameacha kweli kuvuta sigara, tabia ambayo amekiri wazi kuwa amekuwa akipambana nayo siku za nyuma.
Khan, ambaye wakati mmoja alivuta hadi sigara 100 kwa siku, amesema kuachana na jambo hilo ni hatua kubwa kwake na ni zawadi yake kwa mashabiki zake siku yake hiyo ya kuzaliwa.
Shah Rukh Khan amefafanua juu ya safari yake ya kuacha kuvuta sigara, akielezea hamu yake ya kuboresha afya. “Nilifikiri ningehisi kukosa pumzi baada ya kuacha kuvuta sigara, lakini bado ninajisikia vizuri,” amesema.
Shah Rukh katika hafla hiyo pia amepongezwa na familia yake. Binti yake, Suhana Khan, Mkewe, Gauri Khan pia baadhi ya mastaa walioshiriki ni Kareena Kapoor Khan, Ananya Panday, Kamal Haasan, Farah Khan na Vicky Kaushal wakituma salamu zao za dhati kwa mwigizaji huyo mpendwa.