Muziki

Serikali kutambulisha muziki wa singeli kimataifa

DAR ES SALAAM:SERIKALI ya Tanzania imeanza juhudi za kuutambulisha muziki wa Singeli kimataifa kwa kutaka uorodheshwe kama urithi wa utamaduni usioshikika katika Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO).

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, ametangaza azma hiyo wakati akifungua warsha ya Uteuzi wa Urithi wa Utamaduni Usioshikika iliyoandaliwa na UNESCO katika hoteli ya Sheraton, jijini Dar es Salaam.

Msigwa alieleza kuwa muziki wa Singeli una uwezo mkubwa wa kuchochea maendeleo na kuleta umoja katika jamii ikiwa utazingatia maadili na kuakisi utambulisho wa taifa.

Alisisitiza kuwa tafiti zilizofanywa na wataalamu wa vyuo vikuu, akiwemo Dkt. Kedmon Mapana, zimebaini kuwa Tanzania ndiyo chimbuko la muziki wa Singeli duniani.

Katika warsha hiyo, Msigwa aliitaka Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), chini ya uongozi wa Katibu Mtendaji Dkt. Kedmon Mapana, kuhakikisha linasimamia kikamilifu maadili katika muziki wa Singeli ili kuufanya uwe na hadhi inayostahili mbele ya dunia.

Warsha hiyo ya siku mbili ilikusanya wadau mbalimbali wa muziki, viongozi wa serikali, na wataalamu wa utamaduni, ikiwa na lengo la kuweka msingi thabiti wa kutambulika kwa muziki wa Singeli kimataifa na kuendelea kuufanya kuwa daraja la kuunganisha watu na kukuza utamaduni wa Tanzania.

Msanii maarufu wa Singeli, Seleman Jabiri, anayejulikana kwa jina la Msaga Sumu, aliishukuru serikali kwa kuupa kipaumbele muziki wa Singeli na kuutambua kama alama ya utambulisho wa taifa.

Related Articles

Back to top button