Serikali kulisaidia Tamasha la ZIFF

ZANZIBAR: SERIKALI itaendelea kuiunga mkono na kulilinda Tamasha la Kimataifa la Filamu la Zanzibar (ZIFF) lisipotee kwa kuwa lina umuhimu mkubwa katika utamaduni na uchumi wa nchi.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Thabit Kombo wakati akihutubia hadhara kwenye usiku wa tuzo za Tamasha hilo.
Katika usiku huo uliorushwa moja kwa moja na televisheni ya Azam tuzo nyingi zilienda kwa taifa la Uganda.
Alisema Wizara anayoiongoza itafanya kikao maalum na ZIFF, na itawaalika mabalozi wa nchi kadhaa kujadili suala la filamu na sanaa, akisisitiza kuwa ni suala la kipaumbele. Lengo ni kuhakikisha milango inafunguka na fursa zaidi zinapatikana kwa tasnia hii.
Waziri Kombo alibainisha umuhimu wa jukwaa la ZIFF na majukwaa mengine katika kuchangia uchumi wa nchi, akitolea mfano wa Misri yenye matamasha 57 kila mwaka ambayo ni sehemu muhimu ya uchumi wao.
Alihimiza sekta binafsi kuona fursa kubwa iliyopo katika tasnia ya filamu.
Waziri Kombo alikumbushia jinsi filamu zinavyoweza kuleta mabadiliko makubwa, akibainisha kuwa marais wawili wa Tanzania, Dk Samia Suluhu Hassan na Dk Hussein Mwinyi, wameonesha mfano kupitia Royal Tours zao, ambazo zimekuwa maarufu sana duniani kupitia filamu. Hii inaonesha jinsi filamu zinavyoweza kutumika kukuza utalii na diplomasia ya nchi.
“Kama China inaleta watalii kibao kutokana na uigizaji uliofanywa na viongozi wetu wa kitaifa Rais Samia Suluhu Hassan katika Royal Tour na Dk Hussein Mwinyi,sekta binafsi ni vyema ikashiriki kwa sapoti,” alisema Kombo.
Aidha Waziri Kombo alifafanua kwamba ZIFF imekuwa kitalu cha kuzalisha vipaji vingi vikubwa. Akimtaja Joseph Mwale kama mfano halisi aliyezaliwa na ZIFF na leo ni CEO, wa taasisi hiyo.
Aliongeza kuwa tamasha hili limezalisha vipaji vingi vilivyochukuliwa hata Bara chini ya uongozi wa Dk Samia. Alisisitiza kuwa “ZIFF kama shule imefundisha wengi sana, ni shule ya kimataifa,” akihimiza matumizi ya wakongwe na wahadhiri kama Prof. Martin Mhando kuwasaidia vijana.
Katika tamasha hilo, Ofisa Mtendaji Mkuu Joseph Mwale alisema kwamba tamasha mwakani litazungumzia AI na Hadithi zetu.