
KIGOMA: RAIS wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania ‘TFF’, Wallace Karia ameweka wazi licha ya kutoa elimu kwa waamuzi juu ya matumizi ya teknolojia ya usaidizi wa muamuzi kwa njia ya video VAR, matumizi yake hayataanza kutokana kutokuwa na miundombinu bora ya viwanja.
Karia ambaye ni Mgeni rasmi katika mkutano mkuu wa 11 wa Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB), ambo umefanyika katika ukumbi wa Lake Tanganyika, Kigoma amesema mafunzo yakiwa kamili wanaweza kuanza matumizi ya VAR lakini miundombinu inawapa ugumu wa kutumia kwa mwa msimu huu.
“Hatuna miundombinu bora ya viwanja ambavyo vinaweza kuruhusu kutumia VAR katika kila mechi za Ligi Kuu Tanzania, tukifanikiwa kuweka sawa basi tutaanza kutumia.
Tunaongea na Shirikisho la Soka Duniani FIFA kuanza kupata VAR za bei nafuu ambazo zinalingana na miundo mbinu yetu, hatusemi ni lini tunaweza kutumia lakini ndani ya miaka miwili hii tunaimani itakuwa vizuri,” amesema.
Karia amesema kuwepo kwa VAR kunapunguza malalamiko kwa makocha na wadau wa soka kwa makosa ya kibinadamu yanayofanywa na waamuzi wetu katika michezo ya ligi.