Burudani

Rehema Semfukwe kupamba Super Sunday KKKT Mabibo

DAR ES SALAAM: Mwimbaji mashuhuri wa nyimbo za Injili Tanzania, Rehema Semfukwe, anatarajiwa kuwa miongoni mwa waimbaji watakaopamba Tamasha la Vijana la Kusifu na Kuabudu lijulikanalo kama “Super Sunday”, litakalofanyika Julai 13, 2025 katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Mabibo External.

Akizungumza na Spoti Leo, Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Usharika huo, Erick Kisaule, amesema tamasha hilo ni sehemu ya ibada maalum ya vijana yenye lengo la kuwaunganisha na kuwaelekeza katika njia za kumcha Mungu.

“Tamasha hili lina malengo makubwa: kuwaunganisha vijana, kuwapa nafasi ya kusifu na kuabudu pamoja, kujifunza neno la Mungu na kubadilishana mawazo ya kujenga,” amesema Kisaule.

Ameongeza kuwa shughuli hiyo pia inalenga kuwaepusha vijana na vishawishi vya mitaani visivyofaa kama matumizi ya dawa za kulevya, wizi na matendo mengine maovu.

“Hakutakuwa na kiingilio, kila mtu anakaribishwa. Kutakuwa na michezo mbalimbali, chakula, kucheza na kusifu – ni siku ya kipekee isiyopaswa kukoswa,” amesisitiza Kisaule.

Katika wiki ya tamasha hilo, mnamo Julai 6, kutakuwa na mechi ya kirafiki ya mpira wa miguu baina ya vijana wa Usharika wa Mabibo External na Usharika wa Kisukuru kama sehemu ya maandalizi ya Super Sunday.

Kwa upande wake, mwimbaji Rehema Semfukwe ametoa wito kwa vijana kujitokeza kwa wingi akisema, “Tuwe tayari kwa ibada ya kipekee ya kumsifu na kumtukuza Bwana. Mungu ana jambo kubwa kwa kizazi hiki.”

Tamasha hilo pia litashirikisha waimbaji wengine kama Obby Alpha na vikundi vya uimbaji vya kanisa hilo, huku likiwa wazi kwa watu wa rika zote.Mahali: KKKT Usharika wa Mabibo External, Julai 13, 202, Kuanzia saa 3:00 asubuhi Karibu wote kwa ibada ya kipekee ya vijana.

Related Articles

Back to top button