Real Madrid yafikia makubaliano ya awali kumsajili kinda wa Manchester United

MADRID: KLABU ya Real Madrid ina matumaini makubwa ya kumnasa mshambuliaji chipukizi wa Manchester United, JJ Gabriel, baada ya kufikia makubaliano ya mdomo na mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 16.
Gabriel bado amesajiliwa na Manchester United, lakini hajarudi katika klabu hiyo tangu alipoondoka mwezi Septemba mwaka huu.
Nyota huyo chipukizi alikuwa akitarajiwa kuweka historia kwa kuwa mchezaji mwenye umri mdogo zaidi kucheza mechi rasmi ya Manchester United, katika mchezo wa Kombe la Carabao dhidi ya Brighton mwezi Septemba.
Hata hivyo, aliamua kutafuta fursa nyingine ya kucheza soka la wakubwa na kwa sasa amekuwa akifanya mazoezi binafsi nchini Hispania.
Hali hiyo imevutia vilabu mbalimbali barani Ulaya, vikiwemo Barcelona na Paris Saint-Germain, lakini Real Madrid sasa inatarajia kukamilisha usajili wake katika dirisha la usajili la Januari.
Kwa mujibu wa taarifa za BBC Sport, vyanzo vya habari vimedokeza kuwa Real Madrid imefikia makubaliano ya mdomo na Gabriel pamoja na wawakilishi wake, ingawa mazungumzo rasmi kati ya vilabu hivyo viwili bado hayajaanza.
Gabriel alijipatia umaarufu mkubwa baada ya kufunga mabao matatu katika mchezo wake wa kwanza wa UEFA Youth League.
Pia alitunukiwa tuzo ya mchezaji bora wa Ligi ya Vijana chini ya miaka 18 ya Premier League msimu uliopita, licha ya kuwa na umri wa miaka 14 pekee wakati wa msimu huo.
Mchezaji huyo pia amepata pasipoti ya Umoja wa Ulaya (EU), hatua inayotarajiwa kurahisisha uwezekano wake kusajiliwa na klabu nje ya England.
Manchester United inatarajiwa kupata fidia iwapo Gabriel ataondoka, ingawa kiasi hicho kitakuwa kidogo zaidi iwapo atajiunga na klabu isiyoshiriki Premier League.
Chanzo kimoja ndani ya Manchester United kilimtaja Gabriel kuwa miongoni mwa vipaji bora vya soka la vijana barani Ulaya.
Aliyekuwa kocha mkuu wa muda wa United, Darren Fletcher, pia aliwahi kueleza kuwa mchezaji huyo ana uwezo mkubwa wa kufikia mafanikio makubwa katika soka.
Akizungumzia hali ya Gabriel baada ya United kufungwa na Brighton katika Kombe la EFL, kocha Michael Carrick alisisitiza umuhimu wa kulinda ustawi wa wachezaji vijana.
Carrick alisema klabu inapaswa kuwa makini kuhusu ustawi, maendeleo na mazingira yanayowazunguka wachezaji wake chipukizi.
Kwa sasa, macho yanaelekezwa Januari huku Real Madrid ikitarajia kukamilisha dili hilo na kupata huduma ya mmoja wa vijana wanaotajwa kuwa na kipaji kikubwa katika soka la Ulaya.




