Africa

Ramovic: Kesho tutawasha moto kwa Mkapa

DAR ES SALAAM: HATMA ya Yanga kufuzu hatua ya robo fainali Ligi ya Mabingwa Afrika, itajulikana Jumamosi, Januari 18, katika mchezo wa mwisho hatua ya makundi utakaochezwa Uwanja wa Benjamini Mkapa dhidi ya MC Alger.

Yanga watashuka dimbani kusaka alama tatu ili kupata ya kufuzu,wakati MC Alger wanahitaji ushindi au sare ili kufuzu inayofuata.

Kuelekea mchezo wa kesho, Kocha Mkuu wa Yanga, Sead Ramovic, amesema wanatambua umuhimu wa mchezo, kwao na wapinzani wao wanahitaji nini. Ana matumaini makubwa kutokana na namna wachezaji wake wanajitoa na kuelewa mfumo wake.

“Kesho tunakwenda kujitoa kwa kila iwezekanalo kulipuka kama moto kuhakikisha tunaweka utawala katika mchezo huo, hatujawahi kwenda kucheza kwa ajili ya sare, lengo letu ni ushindi.

“Sina haja ya kuongelea kuhusu matokeo mengine zaidi ya ushindi hapo kesho, nina wachezaji ambao wanaweza kubadilika kutokana na mbinu zangu au kutokana na mfumo wa wapinzani, sina mashaka na mbinu kwenye kupata matokeo ya ushindi,” amsema.

Kocha huyo ameeleza kuhusu kurejea kwa Maxi Nzengeli na Clatous Chama, amesema Maxi mchezaji wa ajabu, bado hawajawa sawa kucheza hapo kesho, Chama amerejea, wataangalia mwenendo wa kila mchezaji kimwili na kiakili kabla ya kufanya maamuzi.

Nahodha wa Yanga, Dickson Job amesema wapo tayari kwa mchezo wa kesho  wanahitaji matokeo mazuri kuingia katika hatua inayofuata ya robo fainali.

“Tunaelewa umuhimu wa mchezo wa kesho, tunatambua ukifanya kosa moja itakuwa tatizo kubwa, kumaliza mechi nyumbani ni faida kwa sababu tunakuwa karibu na mashabiki zetu,” amesema

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button