Prof Jay: Nimeuona mkono wa Mungu

MKALI wa muziki wa Hip Hop nchini Joseph Haule ‘Professor Jay’ Leo rasmi ameachia wimbo wake mpya na wa kwanza wa shukrani baada ya kupita siku 462 akiwa anapatiwa matibabu Hospitali.
Prof Jay anasema “baada ya kulala kitandani kwa siku 462 na watanzania kunikimbilia, kuniombea na kunichangia. Hakika nimeuona mkono wa Mungu nami nimewapa zawadi ya shukrani ya dhati kwa watanzania kwa kuwaletea wimbo mpya wa Siku 462”.
Professor Jay amesema alikaa ICU siku 127 wakati akielezea matukio mbalimbali aliyopitia mkongwe huyo kipindi chote alipokuwa akiumwa.
Akizungumza na Clouds Fm, Professor Jay amesema ingawa magonjwa ni mawaidha ameshuhudia watu wakipoteza maisha.
“Ingawa magonjwa ni mawaidha watu wanasema, lakini watu wanakufa sana, kwa mimi niliyekaa ICU siku 127, unajua kule ICU watu hali zao mbaya sana, kujikuta ICU na una- survive siku 127 sio mchezo”.
Prof Jay ameongeza kuwa kuugua tatizo la Figo kulifanya afikie hatua ya kutobolewa Koo ili kuondoa uchafu uliokuwa ukisababisha ashindwe kuongea.
Pia ameongeza kuwa, alikuwa akichoma sindano inayogharimu Sh milioni 5 ambapo alitakiwa kuchoma sindano 10.
Tatizo hilo Figo lilifanya apelekwe hadi hospitali iliyopo India, na ndilo lililompa msukumo wa yeye kuanzisha ‘Foundation’ itakayohusika na masuala ya kusaidia Watu wanaosumbuliwa na Ugonjwa huo. Ambapo amepanga kuzindua Novemba 24, 2023.
Wakati huo huo, Makamu Rais wa Professor Jay Foundation, Black Chatta amesema moyo wa Professor Jay ulisimama mara tatu katika vipindi tofauti lakini juhudi za Madaktari zilimnusuru na kifo mkongwe huyo, wakati akielezea matukio mbalimbali aliyopitia Kaka yake kipindi alipokuwa akiumwa.