MasumbwiMichezo Mingine

Pialali atuma salamu kwa Mfaume Mfaume

UKIZUNGUMZIA upinzani mkubwa wa ngumi au dabi yenye nguvu zaidi kwa Dar es Salaam
ni dabi yoyote itakayohusisha mabondia kutoka Mabibo na wale kutoka eneo la Manzese, ambao wote wanatokea Wilaya ya Ubungo.

Kumekuwa na ‘gym’ nyingi eneo la Mabibo, lakini bondia ambaye amekuwa akifanya vizuri zaidi ni kutoka gym ya Naccoz, Mfaume Mfaume chini ya kocha Rama Jah wakati Manzese bondia anayefanya vizuri zaidi ni Iddi Pialali.

Wawili hawa wamekuwa wakifanya vizuri kwenye rekodi za kidunia, ambapo Pialali anashika nafasi ya kwanza kwa Tanzania katika uzito wa Welter akiwa na nyota moja na nusu, huku Mfaume Mfaume akishika nafasi ya tatu katika uzito wa Super Welter iliyoshikwa na Hassan Mwakinyo na Meshack Mwankemwa.

Kila mmoja anafanya vizuri anapokuwa ulingoni kwa nafasi yake ingawa kila mmoja anaamini yeye ni mkali zaidi na Rais wa ngumi wa Ubungo kwa ukanda wa ubungo anayepaswa kuliwakilisha jimbo hilo katika ulimwengu wa ngumi za Tanzania na duniani kwa ujumla.

Katika kuelekea pambano la marudio kati ya Pialali na Mfaume Mfaume Septemba 1, 2023 baada ya kuvunjika usiku wa Desemba 27, mwaka jana, Pialali anasema ni pambano lake linaloenda kumtangaza rasmi kama Rais wa Ngumi Ubungo ikiwemo Manzese na Mabibo kwa ujumla.

Akizungumza na mwandishi wa makala haya, Pialali alisema kwa miaka mingi kumekuwa
na ubishani wa kumtafuta nani anaweza kuipeperusha bendera ya ubingwa wa ngumi Ubungo kutokana na eneo hilo kuwa na mabondia wengi, anasema sasa ubishi huo unaenda kufika mwisho.

Pialali anasema anataka kuwahakikishia Watanzania kwamba pambano lake na Mfaume Mfaume sio kwamba lilivurugika baada ya kupigwa kichwa, ila bondia mwenzake
aliamua kulivuruga ili asitangazwe bingwa.

“Nataka nioneshe jamii kwamba nipo tayari kuonesha kwamba, mimi ni bondia mzuri na nani hasa bingwa katika ukanda huu wa Ubungo,” alisema.

Anasema katika kuelekea katika pambano lake na Mfaume Mfaume, tayari amejiandaa kwa mazoezi makali, ikiwemo pambano lake la juzi na bondia Simon Ngoma kutoka nchini
Zambia.

“Niliwaambia sitaki bondia kiazi, nahitaji mtu ambaye naweza kupigana naye na kila mtu akajua kwamba mimi nimepambana na ushindi nimepata kihalali. “Ushindi huu na Ngoma
ni salama kwa Mfaume katika marudio yetu, kwamba ajiandae na siwezi kumuacha
salama,” anasema.

Kumpiga bondia Ngoma sio kazi rahisi kwa kuwa sio mgeni kwa ngumi za Tanzania, alishawahi kuja katika pambano lake na bondia Ibra Classic, ambaye aliondoka na ushindi
ndiyo  maana imekuwa rahisi kwake kuja kupigana tena.

Pialali anasema katika mapambano yake aliwahi kukutana na mapambano magumu zaidi kama ambalo alipambana na bondia kutoka Thailand, Arne Tinampey, ambaye alimsumbua Hassan Mwakinyo, lakini aliibuka na ushindi.

Bado anasema alikutana na mapambano mengine na kufanya vizuri kama pambano lake na bondia kutoka Afrika Kusini, Tulani Mbenge na pambano lake la ndani ya nchi na Twaha Kiduku ambapo yote aliibuka na ushindi.

“Mapambano ambayo niliyapata mimi, hata Mfaume mwenyewe asingeweza kutoka. Lakini nimepambana na nimetoka na ushindi, hivyo kwake naona kama vile napita tu,” alisema.

Lakini pia akigusia mapambano yake ya nje ya nchi, anasema mapambano ya kimataifa kwa sasa yamebadilika sana, kwa kuwa kipindi ambapo alikuwa anaenda kupambana nje ya nchi kwa miaka ya nyuma kulikuwa na changamoto ya muda.

“Ulikuwa unapangiwa ndani ya wiki mbili kwenda kupambana, unajikuta hujafanya mazoezi ya kutosha wala hujui ni nani hasa unaenda kupambana naye,” anasema.

Anasema lakini kibaya zaidi kwamba hata pambano lenyewe limeandaliwa na kampuni
ambayo ndiyo bondia wake anaenda kupambana naye hivyo kushindwa ilikuwa ni nadra sana.

Kwa sasa hivi anasema mapambano yamebadilika sana kwa bondia kupewa kwa zaidi ya miezi mitatu kujiandaa, hivyo unayo nafasi hata ya kumsoma bondia wako kupitia mitandao ya kijamii au rekodi yake.

Anasema zamani alikuwa akijiandaa na timu yake ya watu wa Manzese lakini kadri ulimwengu wa ngumi umeendelea kupanuka, kwa sasa amejitanua zaidi kwa kutengeneza
timu yake ya ushindi kwa ajili ya mapambano yote ambayo amekuwa akiyapata.

Anasema zaidi ya kuwa na kocha wake ambaye anasimamia mazoezi yake yote, lakini sasa hivi anaye meneja wake ambaye ni Haider Mwarabu, amekuwa mtu ambaye anamshukuru kwa kuendelea kumsogeza mbele katika ngumi zake.

Anasema kwa sasa ana mategemeo makubwa ya kufanya mapambano ya kuweza kuvutia zaidi na kusogea mbele kimataifa, kwa kuwa anaamini mchezo wa ngumi ni miongoni mwa mchezo pendwa hivyo hiyo siku atanufaika na mchezo huo.

Related Articles

Back to top button