Palmer aoga sifa za Maresca

EAST RUTHERFORD, KOCHA wa mabingwa wapya wa Dunia Chelsea, Enzo Maresca, amesifu uwezo wa Kiungo mshambuliaji wake Cole Palmer wa kuinua kiwango chake kilichomuwezesha kufanya vizuri kwenye fainali na kuchaguliwa kuwa mchezaji bora wa michuano hiyo iliyotamatika kwa ushindi wao wa mabao 3-0 dhidi ya Paris St Germain na kutwaa kombe hilo.
Maresca aliwaambia waandishi wa habari Palmer ni mchezaji mzuri wa michezo ya maamuzi kama huo wa fainali baada ya Palmer kufunga mara mbili na kutoa asisti kwa Joao Pedro katika ushindi huo uliowapa taji mbele ya mabingwa wa Ulaya PSG.
“Hizi ndizo mechi tunazotarajia Cole Palmer kuonekana na kwa mara nyingine tena alionesha kile tulichomzoea. Ni mzuri sana kwenye michezo ya maamuzi” amesema Maresca
Kocha huyo alifichua kuwa mpango wake mkuu ulifanya kazi kwa ukamilifu huku Chelsea wakiikabia juu PSG na kutumia mipira iliyotua moja kwa moja nyuma ya safu ya ulinzi ya wapinzani wao na kuleta madhara huku wakitumia upande wa kushoto wa PSG uliotetereka muda wote wa kipindi cha kwanza.
“Wazo lilikuwa ni kwenda ‘man to man’ kwa sababu ukiwaachia nafasi PSG watakuua, hivyo tulijaribu kuwafanyia fujo na kuwakosesha pumzi mapema na nguvu hiyo ilikuwa muhimu katika dakika 10 za kwanza kutokana na joto kali ilikuwa ni hali ngumu sana” Maresca alieleza.
Maresca aliwasifu wachezaji wake kwa kutumia vyema mpango wa mchezo aliokuwa nao akilini, huku mbinu yao ya hali ya juu ikithibitika kuwa thabiti katika hali ya hewa ya New Jersey, akisema kwamba anafuraha kushinda Kombe la Dunia la Klabu ambalo anadhani litakuwa bora siku zijazo.