Osama aahidi kumakalisha Mazome

DAR ES SALAAM: BONDIA kutoka Mtwara, Osama Alabi, ambaye ameweka kambi yake ya maandalizi Mazense ametangaza kumkalisha mpinzani wake Ally Mazome wa Morogoro kwa TKO katika pambano la Boxing on Boxing Day litakalofanyika Desemba 26, 2025 katika Ukumbi wa Warehouse, Masaki.
Akizungumza m Dar es Salaam , Alabi anayefahamika pia kama Osama Korosho amesema amejipanga vizuri kuhakikisha anapata ushindi katika pambano hilo akisisitiza kuwa mashabiki wa Mtwara na Watanzania kwa ujumla wawe sehemu ya “historia mpya” ambayo anatarajia kuiandika ulingoni.
“Nimejiandaa vya kutosha, naimani hii ndiyo siku yangu. Naomba mashabiki wangu wote wa Mtwara na Watanzania waje kushuhudia ushindi wa kihistoria,”alisema.
Kwa upande wa mashabiki wake, wameeleza kujiamini kuwa Osama ataibuka na ushindi mnono wakifananisha uwezo wake na “paka aliyekula mboga ya familia.”
“Tumejiandaa, Osama anashinda bila shaka,” — Eliud Mwakapala (Shabiki)
“Siku hiyo Osama atapiga kazi, tunasubiri tu,” — Udi Kilale (Shabiki)
Kocha wa bondia huyo, Saburi Shabani, amesema maandalizi yamekamilika na mpiganaji wake yuko kwenye ubora wa juu na hana shaka na ushindi.
Katika mfululizo wa mapambano ya siku hiyo, bondia nyota Hassan Mwakinyo ataiwakilisha Tanzania kwenye pambano maalum, huku Hamadi Furahisha akitarajiwa kupanda ulingoni dhidi ya Mmalawi Hanock Phiri. Wengine watakaopambana ni Ally Ngwando na Mussa Makuka.
Kwa upande wa wanawake, bondia Debora Mwenda atachuana na Mmalawi Mariam Dick katika pambano linalotarajiwa kuvutia mashabiki wengi.




