Kwingineko

Ortega aitwa Ujerumani kwa mara ya kwanza.

FREIBURG: Mlinda mlango namba mbili wa mabingwa watetezi wa ligi kuu ya England Manchester city Stefan Ortega ameitwa kwa mara ya kwanza kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Ujerumani kinachoingia kambini kujiandaa na mechi za kombe la mataifa ya Ulaya (UEFA Nations League).

Ortega mwenye miaka 32 ameitwa katika kikosi cha timu hiyo sambamba na mlinda lango wa Stuttgart Alexander Nuebel na Oliver Baumann kutoka katika klabu ya Hoffenheim, hii ni kufuatia golikipa namba moja wa kikosi hicho na FC Barcelona Marc-Andre Ter Stegen kukosekana kutokana na jeraha la goti.

Ujerumani itakuwa mwenyeji wa wa Bosnia and Herzegovina Novemba 16 mwaka huu mjini Freiburg kisha kusafiri hadi Budapest kukipiga dhidi ya timu ya taifa ya Hungary siku tatu baadaye. Hata hivyo taifa hilo babe kwenye soka duniani lilishafuzu robo fainali ya michuano hiyo, baada ya sare 1 na ushindi kwenye mechi 3.

“Tulishafika robo fainali, tena kwa kuwahi, sasa tunataka kuongoza kundi letu ikiwezekana mbele ya mashabiki wetu kwenye uwanja wa nyumbani wa Freiburg” Nagelsmann amewaambia waandishi wa habari

Pamoja na Ter Stegen Ujerumani wataendelea pia kuwakosa fowadi wa West Ham Niclas Fullkrug, Jamie Leweling wa Stuttgart, kiungo wa Bayern Aleksander Pavlovic, winga Leroy Sane na kiungo David Raum wa RB Leipzig.

Related Articles

Back to top button