
MTENDAJI Mkuu wa klabu ya Azam Abdulkarim Amin ‘Popat’ amesema klabu hiyo inafikiria kumpa mkataba wa kudumu kocha wa sasa Kally Ongala kutokana na mwenendo mzuri tangu akabidhiwe timu hiyo.
Akizungumza na SpotiLeo kiongozi huyo amesema bodi ya timu hiyo ipo kwenye mjadala kuhusiana na mchakato huo wa kumpa Ongala mkataba wa kudumu.
“Ni kocha mzuri kwa kweli na amethibitisha hilo kwa matokeo yake anayoendelea kuyapata kwenye ligi kitu ambacho ndiyo tulikuwa tunakihitaji kwa muda mrefu,” amesema Popat.
Amesema kipindi hiki ambacho wanapokea maombi suala la kocha huyo litakuwa moja ya ajenda zao na kama watakubaliana watamkabidhi kocha huyo jukumu hilo.
Tangu Kally akabidhiwe jukumu la kukinoa kikosi cha Azam, timu hiyo imeshinda mechi zote sita na kuiweka timu hiyo nafasi za juu katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania bara.