Ofweneke afurahishwa binti yake kuiwakilisha Kenya

NAIROBI: MUANDAAJI na mtangazaji wa kipindi mashuhuri cha ‘Hero Mr Right’ Kenya, Sande Bush maarufu kwa jina la Dk. Ofweneke, hivi majuzi alichapisha tukio la kufurahisha ambalo limeteka mioyo ya wengi kwenye mitandao ya kijamii.
Binti yake aitwaye Faith, mwanafunzi mahiri Darasa la 9, aliiwakilisha Kenya katika shindano la kifahari la Mjadala wa Afrika Mashariki.
Dk. Ofweneke, alishindwa kuzuia majivuno yake alipoandamana na bintiye hadi uwanja wa ndege, na kisha kupiga naye picha huku akiandika maneno ya kujikweza kutokana na mafanikio ya binti yake huyo jambo lililogusa hisia za wengi.
Katika picha hiyo, Faith aling’ara pembeni ya baba yake, akiwa tayari kwa safari yake, huku Dk Ofweneke akimkumbatia kwa uchangamfu, upendo huku akionyesha majigambo yake kwa njia ya uchekeshaji.
Mchekeshaji huyo aliingia kwenye mitandao ya kijamii kueleza hisia zake za dhati, akitafakari jinsi ilivyokuwa ajabu kwa bintiye kuanza safari ya kimataifa akiwa na umri wa miaka 15 pekee.
“Kama wazazi, tumaini letu kuu ni kwamba watoto wetu wanatuzidi. Ninajivunia sana,” Dk. Ofweneke aliandika, akijumuisha maoni ya wazazi wengi wanaotamani kuona watoto wao wakifanya vyema zaidi ya mafanikio yao wenyewe.
Watumiaji wa mitandao ya kijamii walijumuika katika maadhimisho hayo, wakimtakia heri. Wengi walimsifu Dk Ofweneke kwa kuwa baba mwema, huku wengine wakishiriki maombi ili akafanikiwe katika shindano hilo.
Katika chapisho linalohusiana, Dk. Ofweneke na mpenzi wake wa zamani, mwimbaji wa nyimbo za injili Nicah the Queen, walisherehekea maendeleo ya kielimu ya binti yao alipopanda daraja hadi Darasa la 9. Wazazi hao wawili walichapisha jumbe tamu na picha ya familia huku binti yao akisimama kwa furaha kati yao.
Faith anapowakilisha Kenya katika shindano la Mjadala la Afrika Mashariki, yeye sio tu anabeba fahari ya familia yake bali pia anajumuisha matarajio ya vijana wengi wa Kenya.