Novak Djokovic kucheza Olimpiki, Paris 2024

Paris, Ufaransa: MCHEZAJI namba moja wa zamani wa tenisi duniani Novak Djokovic atacheza kwenye Michezo ya Olimpiki ya Majira ya joto huko Paris kulingana na taarifa ya Kamati ya Olimpiki ya Serbia.
Novak Djokovic na Dusan Lajovic wametimiza masharti kulingana na viwango vya mashindano hayo na wamethibitisha ushiriki wao katika Michezo ya Olimpiki ya Majira ya joto huko Paris 2024 ingawa Djokovic bado hajathibitisha hadharani kuhusiana na tangazo hilo.
Mwanzoni mwa Juni, mshindi huyo mara 24 wa Grand Slam alijiondoa kabla ya robo fainali ya dhidi ya Casper Ruud kwenye mashindano ya Roland Garros ambapo uchunguzi ulipofanyika aligundulika kuwa na majeraha ya goti lake la kulia.
Wiki mbili zilizopita, Djokovic alithibitisha kuwa alifanyiwa upasuaji kwenye goti lake na kwamba yupo katika hali nzuri lakini hakutoa muda wa kurejea kwake uwanjani.
Djokovic amekuwa akisifia Michezo ya Olimpiki hasa msimu huu wa joto huku akitamani kupata medali ya dhahabu ambayo hakuwahi kuipata ambapo Oktoba mwaka jana, alisema kushinda dhahabu katika Olimpiki ni moja ya matamanio yake makuu.
“Michezo ya Olimpiki ya Paris ni muhimu sana. Michezo ya Olimpiki imekuwa kipaumbele kwangu kila wakati,” Djokovic alisema mnamo Aprili kabla ya pambano lake huko Monte Carlo.
Amecheza katika mashindano manne ya Olimpiki na kushinda medali ya shaba huko Beijing mwaka 2008.
Alipoteza mechi ya medali ya shaba na Juan Martin del Potro mjini London mwaka wa 2012. Alipoteza tena kwa Muajentina huyo miaka minne baadaye katika raundi ya kwanza mjini Rio.




