“Nikosoeni kwa mipaka” – Pulisic

MANHATTAN, Winga wa timu ya taifa ya Marekani na Klabu ya AC Milan ya Italia Christian Pulisic amewajia juu wakosoaji wake wanaodai kuwa hana ‘commitment’ na timu ya taifa baada ya winga huyo kukataa kucheza Kombe la CONCACAF akisema wakosoaji hao wanavuka mipaka
Pulisic, aliyeichezea AC Milan michezo 50 katika msimu uliomalizika, amesema uamuzi wake wa kutocheza michuano hiyo ni kupata muda wa kupumzika na kupata nafuu na ni uamuzi sahihi kwake na kwa timu inayojiandaa kushiriki Kombe la Dunia la mwakani wakiwa wenyeji Pamoja na Mexico na Canada.
Wachezaji nguli wa zamani wa Marekani Landon Donovan na Alexi Lalas ni miongoni mwa waliowakosoa wachezaji walioamua kukacha michuano hiyo na maoni yao hayakumpendeza Pulisic.
“Inapokuja kwa watu kama hao, ni ngumu kwa sababu ni watu niliokuwa nawatazama katika makuzi yangu ya soka ninawaheshimu sana kama wachezaji wakubwa ni ngumu kwa sababu baadhi yao nimekuwa nao pembeni na wengi wananiunga mkono na wanasema tofauti hadharani” kijana huyo wa miaka 26 aliambia podikasti ya CBS Sports Alhamisi usiku.
“Yote kwa yote, unaweza kuzungumzia uchezaji wangu, lakini kuhoji ‘commitment’ yangu kwa timu ya taifa, kwa maoni yangu huko ni kuvuka mipaka.”
Marekani ilipokea kichapo cha nne mfululizo Jumanne iliyopita ilipopoteza kwa mabao 4-0 nyumbani dhidi ya Switzerland katika mechi ya kirafiki. Mbali na Pulisic wachezaji Yunus Musah na Antonee Robinson pia hawatacheza Kombe la CONCACAF linaloanza Juni 14 hadi Julai 6 licha ya kutokuwa majeruhi.